Release No. 017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 6, 2012
Mechi
namba 107 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Villa Squad na Simba
iliyochezwa Februari 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
imeingiza sh. 30,017,000.
Watazamaji
waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo ni 8,698 ambapo kiingilio
kilikuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya
rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B na sh. 15,000 VIP A.
Baada
ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni
sh. 4,578,864.41 fedha zilizobaki zilikuwa sh. 25,438,135.59. Gharama
za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli
ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000.
Posho
ya kujikimu kwa mwamuzi wa akiba sh. 30,000, gharama za tiketi sh.
3,960,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000
na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000. Nyingine ni Jichangie
ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 608,860
wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata
sh. 521,880.
Mgawo
baada ya gharama za awali; uwanja na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kila moja ilipata sh. 1,503,853.56, Mfuko wa Maendeleo
ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 751,926.78, gharama za mechi sh.
1,503,853.56, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 150,385.36, DRFA sh.
601,541.42 na kila klabu ilipata sh. 4,511,560.68.
MUJUNI KUPIGA KIPENGA RWANDA
Mwamuzi
Israel Mujuni wa Tanzania ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo ya Ligi
ya Mabingwa Afrika kati ya APR ya Rwanda na Tusker ya Kenya
itakayochezwa jijini Kigali kati ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu.
Mujuni
atasaidiwa na Samuel Mpenzu na Khamis Maswa kutoka Tanzania wakati
mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo namba 18 atakuwa Louis Hakizimana wa
Rwanda.
Kamishna wa mchezo huo atakuwa Aboubacar Nkejimana kutoka Burundi.
Nayo
Mafunzo ya Zanzibar katika mechi yake ya kwanza katika raundi ya mchujo
ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Muculmana de Maputo ya Msumbiji
itakayofanyika mjini Zanzibar kati ya Februari 17, 18 na 19 mwaka huu
itachezeshwa na waamuzi kutoka Shelisheli.
Bernard
Camille ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati huku akisaidiwa na Steve
Marie na Gilbert Lista. Mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo namba 27
atakuwa Ramadhan Ibada wa Tanzania wakati Kamishna atakuwa Ali Waiswa
kutoka Uganda.
Kwa mujibu wa CAF, timu 13 bora zenyewe zimeingia moja katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu
hizo ni Coton Sport (Cameroon), El Ahly (Misri), Djoliba (Mali), Stade
Malien (Mali), MAS (Morocco), Raja (Morocco), Sunshine Stars (Nigeria),
TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Hilal (Sudan), El
Merrikh (Sudan), EST (Tunisia), ESS (Tunisia) na Dynamos (Zimbabwe).
VIINGILIO UWANJA WA CHAMAZI- AZAM
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanyia marekebisho viingilio vya
mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zitakazochezwa katika Uwanja wa Azam
ulioko eneo la Chamazi, Dar es Salaam.
Viingilio
katika mechi za uwanja huo sasa vitakuwa sh. 1,000 kwa mzunguko na sh.
5,000 kwa jukwaa kuu badala ya vile vya awali vya sh. 3,000 kwa
mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa kuu. Mabadiliko hayo yalianza kwenye
mechi ya jana kati ya Azam na JKT Oljoro.
Hata hivyo, viingilio hivyo havitatumika kwa mechi zitakazohusu mechi ambazo timu za Simba na Yanga zitacheza kwenye uwanja huo.
Powered by Sorecson : Creation de site internet
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments