WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.”
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 29, 2017) alipofanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Amesema Serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kulipakodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao. Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.
“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakin huyu bwana hajafanya hivyo”
Waziri Mkuu amesema kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Amesema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano mazuri iliyopo kati ya Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.
“Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania sasa huu ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja.”
Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na taratibu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU JUMATANO, NOVEMBA 29, 2017.
Comments