Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
NAIBU Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa amefanya ziara katika kivuko cha Kigamboni na kujionea namna mashine mpya za kieletroniki zilivyoweza kufungwa na kumtaka mhandisi aanze kuzifanyia majaribio kabla ya mwaka huu kuisha ili Januari 2018 zianze kutumika.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara yake na kujionea namna wafanyakazi wanavyotoa huduma kwa abiria wanaofika kwa ajili ya usafiri kwa kivuko kutoka Kigamboni na Kivukoni, Naibu Waziri Kwandikwa amesema kuwa amefurahishwa na huduma zinazotolewa na zaidi amezungumza na baadhi ya wananchi na wote wameonekana kufurahishwa.
" Nimezungumza sehemu mbalimbali na kujionea namna watoa huduma wanavyotoa huduma zao kwa abiria na pia nimezungumza na takribani wananchi kumi wanaotumia usafiri wa kivuko na wote wameonekena kufurahishwa na huduma zenu ,"alisema Naibu Waziri Kwandikwa.
Katika ziara yake ameweza kuzungumza na wahudumu wanaokatisha tiketi na kuwauliza changamoto wanazokutana wakati wa ukatishaji tiketi, ametembelea na kupanda kivuko cha MV KAZI ambacho ni kipya pamoja na kuona namna Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA) wanavyofanya shughuli zao za kila siku.
Amesema, kama serikali wanahakikisha watumiaji wa kivuko hicho wanapata huduma bora na zinazostahili ikiwemo usalama wa safari zao za kila siku.
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akizungumza na mhudumu wa kukata tiketi katika kituo cha Kivukoni wakati alipofanya ziara kuangalia namna abiria wanavyopata huduma zao, juu akikata tiketi ya kuingia ndani.
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake katika kivuko cha Kivukoni na Kigamboni na kujionea uendeshaji wa huduma bora kwa abiria kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA).
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akizungumza na Mhandisi wa kivuko Ally Daudi na akipewa maelezo ya maendeleo ya vivuko vyote vilivyopo chini ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA).
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akikagua mashine za kieletroniki za tiketi zilizofungwa katika Kivuko cha Kigamboni na Kivukoni wakati wa ziara yake iliyofanyika leo Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wananchi wakizungumzia baadhi ya kero ndogo ndogo wanazokutana nazo pia huduma bora wanazozipata.
Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akiwa ziarani katika kivuko cha Kivukoni na Kigamboni iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Picha zote na Zainab Nyamka.
Comments