URAFIKI WA KUPEANA WAKE WASHAMIRI BARANI AFRIKA
picha na mtandao
UKISTAAJABU ya Musa,
utaona ya Firauni. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea mila na desturi zilizopitiwa
na wakati ambazo bado zingalipo barani
Afrika, hasa maeneo ambayo jamii ndogo ndogo zinaishi kwa kujitenga na
nyinginezo.
Miongoni mwa mila hizo
ni zile za kubadilishana wake, vitendo ambavyo ni maarufu miongoni mwa makabila
ya Namibia.
Hata hivyo, haviko
Namibia pekee bali kwa namna nyingine viko katika baadhi ya jamii kama za
Nigeria na vimeshamiri kwa namna tofauti Ulaya hadi kuambukiza mataifa mengine
ya Asia kama vile India.
Namibia iliteka vichwa
vya habari wakati mbunge mmoja alipotaka mila hiyo iwe sehemu ya sheria za
nchi.
Hilo lilizua mjadala
kuhusu haki za wanawake na uhalali wa kuiendeleza katika jamii ya kisasa.
Ikijulikana kama lugha
ya kwao “okujepisa omukazendu,” yaani ‘kumtoa ofa mke kwa mgeni’ haikuwa ikifahamika
nje ya jamii hizo, ambazo idadi yao haifiki
watu 100,000.
Ni aina ya makubaliano
ya kiungwana ambayo marafiki wanabadilishana wake zao bila kikwazo chochote.
Katika hili, ni wazi
wake hawana usemi kupinga suala hilo. Badala yake hubadilishwa, na kuzunguka
baina ya wanaume tofauti tofauti katika nchi, ambayo kuna moja ya viwango vya
juu kabisa vya maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Lakini makabila ya
Ovahimba na Ovazimba yanayoishi kwa kuhama hama hutetea mila yao hiyo yakisema
inaimarisha urafiki na kuzuia uzinzi.
“Ni utamaduni ambao
unatengeneza umoja na urafiki,” alisema Kazeongere Tjeundo, Mbunge na Makamu wa
Rais wa chama cha upinzani cha Democratic Turnhalle Alliance of Namibia (DTA ).
“Ni juu yako kuchagua
miongoni mwa wenzako nani unamruhusu alale na mkeo,” anasema Tjeundo, ambaye
anatokana na kabila la Ovahimba.
Tjeundo amekuwa mstari
wa mbele kushinikiza sheria ya kubadilishana wake tangu alipotangaza kutetea
kiti chake cha ubunge kuelekea uchaguzi wa Novemba 2014.
Ikiwa inatumika zaidi
katika eneo la Kunene la Kaskazini Magharibi karibu na mpaka wa Angola,
makabila hayo kwa kiasi kikubwa yamejitenga na sehemu kubwa iliyobakia ya nchi.
Makabila hayo yamekuwa
yakipuuza kuingia katika maisha ya kisasa, wakifuga mifugo na kuabudu mizimu.
Kutokana na wasiwasi
kuwa VVU inaweza kutumika katika kile alichokiita kuwa kisingizio cha kusitisha
mila yao hiyo ya kale, mbunge huyo wa Jimbo la Opuwo Vijijini na wenzake
wanatafuta namna ya kuifanya kuwa salama zaidi.
Wengi katika makabila
hayo bado wanaishi katika vibanda vya matope na miti na wanaume kwa wake
hutembea wakiwa vifua wazi.
Wanawake huvaa sketi
fupi za ngozi ya mbuzi na vikorokoro vingine vingi kiunoni, shingoni, miguuni
na mikononi huku wakipaka ngozi zao tope la kujikinga na jua.
Tofauti na mataifa au
sehemu nyingine ikiwamo Ulaya, ambako kitendo hicho hufanyika kwa ajili ya
starehe, wahusika hukutana vibandani mwao, ambapo mume au mke wa kundi lingine
hutokomea katika vibanda tofauti wakati wa kubadilishana.
Wanawake hawawezi
kupinga kulala na mwanamume aliyechaguliwa na waume zao, kitu
kinachowakasirisha wanaharakati kama Rosa Namises ambaye anasema kitendo hicho
ni ubakaji wa hali ya juu.
“Kitendo hicho
hakinufaishi wanawake bali wanaume ambao wanataka kudhibiti wenzi wao pamoja na
kuridhisha tamaa za miili yao,” alisema Namises, mbunge wa zamani ambaye
anaongoza taasisi isiyo ya kiserikali ya utetezi wanawake iitwayo Woman
Solidarity Namibia.
Makundi mengine kama
vile Namibia’s Legal Assistance Centre (LAC), kituo cha sheria kilichoapa
kulinda haki za Wanamibia wote, kimepinga uwepo wa mila hiyo katika nchi ambayo
asilimia 18.2 ya wakazi wake milioni 2.1 wanaishi na VVU, kwa mujibu wa takwimu
za taifa hilo.
“Ni kitendo
kinachowaweka wanawake katika hatari ya kiafya,” alisema Amon Ngavetene, ambaye
anasimamia miradi ya Ukimwi ya LAC. Alisema kwamba kiuhalisia wanawake wengi
wanapinga kitendo hicho na wangependa kiharamishwe.
Lakini Kambapira Mutumbo
(40), anasema anajisikia vizuri na mila hiyo na kwamba amekuwa akilala na marafiki
za mumewe bila matatizo.
“Nimefanya mara nyingi
na sina tatizo na mila hii. Ni nzuri kwa sababu ni sehemu ya utamaduni wetu.
Kuna haja gani sasa ya kuibadili?” alihoji.
Cloudina Venaani, mchambuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Mipango ya Maendeleo (UNDP) nchini Namibia, anaamini wanawake hawaipendi mila
hiyo ila wanavumilia tu kwa sababu wanahofia kuwakosea waume zao.
Wenyeji hata hivyo
wanasisitiza kuwa mila hiyo haikiuki haki za wanawake, wakidai wanawake pia
wako huru kuchagua wanawake wa kulala na waume zao – hata kama inatokea kwa
nadra.
Wanasema waume kwa wake
wengi wa Namibia na duniani kwa ujumla wanatoka nje ya ndoa kwa siri, wakati
wao hufanya kwa uwazi na kuondoa hofu na wasiwasi wa kukamatwa.
Na mbunge wa Tjeundohe,
Uziruapi Tjavara, ambaye ni chifu wa Mamlaka ya Jamii ya Otjikaoko katika Mkoa
wa Kunene, anataka mila iendelee lakini ikiendana na elimu ya Ukimwi.
Nchini Nigeria pia
kunaaminika wanawake wa Benue hupewa wageni wa kulala nao kama sehemu ya
starehe. Ijapokuwa watu wengi kutoka jimbo la Benue wamekuwa wakikana madai
hayo, lakini wachache wako wazi kukiri hilo.
“Shangazi yangu ana
rafiki hapa Lagos, ambaye anatokea katika Jimbo la Benue. Siku moja, shangazi
yangu alimfuma akifanya mapenzi na mwanaume mwingine wa Benue na alikasirika
sana, “ anasimulia shuhuda mmoja na kuendelea;
“Mwanamke huyo
alimueleza shangazi kuwa mbona hilo ni suala dogo kama ilivyo kwa utamaduni wao
na kuwa hata mumewe anatoka na mke wa mwanaume huyo.”
Lakini pia kama
utadhani vitendo hivyo viko Afrika tu utakuwa umekosea kwani vimeota mizizi
katika mataifa ya magharibi ambako kunaongoza duniani kwa kila aina ya anasa.
Baba lao inasemekana ni
Italia, ambako inakadiriwa wenzi 500,000 na hata zaidi ya milioni mbili mara
kwa mara hushiriki vitendo vya kubadilishana wake zao.
Hubadilishana rasmi
katika vilabu binafsi vya ngono, huku maelfu zaidi wakifanya vitendo hivyo
katika maeneo ya maegesho ya magari, ufukweni na hata makaburini.
Pia iliripotiwa
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio
Berlusconi aliwahi kutania kuwa alijaribu kumkuwadia mkewe Veronica kwa
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Denmark Anders Fogh Rasmussen.
“Rasmussen ni waziri
mkuu mzuri zaidi Ulaya. Nadhani nitamtambulisha kwa mke wangu kwa sababu yeye
yu mzuri zaidi kuliko Cacciari,” Berlusconi alisema akirejea tuhuma ambazo
mkewe alizikana kuwa alivutiwa na meya wa zamani wa Venice, Massimo Cacciari
Chanzo:Makala za Kimataifa
Comments