KLABU ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imesema msimu huu imedhamiria kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na baada ya mwanzo mzuri wanataka kuendeleza kasi.
Meneja wa Azam FC, Philipo Alando ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba hadi sasa wanajivunia mwenendo wao katika Ligi Kuu, wakiwa hawajapoteza mechi.
Hayo yamesemwa na Alando, ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo, amesema kwamba mashabiki na wapenzi wa Azam wanapaswa kuwa watulivu na kuendelea kuisapoti timu yao.
“Mimi wito wangu kwa mashabiki wa Azam FC ni kwamba huu ni msimu ambao watarajie jambo lolote linaweza likatokea kwa sababu tumekwishaonyesha mwanga kwamba wapi tunaelekea, katika mechi tisa ambazo mwenendo ni mzuri na hatujapoteza mechi hata moja,”amesema Alando.
Meneja huyo amewataka pia mashabiki hao kuendelea kuwavumilia wachezaji wapya chipukizi waliosajiliwa na kupandishwa kikosi cha kwanza cha msimu huu.
“Kwa hiyo tunasisitiza kwamba watuvumilie, waendelee kuwavumilia wachezaji wao wawaamini vijana, kwani watakuja kufanya jambo ambalo litawafuta machozi, ambayo yamekuwa kwenye klabu kwa muda mrefu sasa,” alisema.
Azam FC kwa sasa inazidiwa kwa wastani wa mabao tu na Simba SC wanaoongoza Ligi Kuu, timu zote zikiwa na pointi 17 baada ya mechi tisa, wakifuatia na Yanga na Mtibwa Sugar zenye pointi 17 kila moja.
Baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inatarajiwa kurejea wikiendi hii na Ijumaa Singida United wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua, wakati Azam FC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Jumamosi Uwanja wa Saba Saba.
Azam FC wana taji moja tu la Ligi Kuu kwenye kabati lao, walilotwaa mwaka 2013-2014 baada ya kupanda msimu wa 2008-2009.
Mechi nyingine za Jumamosi, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United n Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Maji Maji na Mbao FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati Jumapili Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Comments