Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana na mawaziri wanne kutoka nchini Uganda ambao wamewasili nchini Tanzania kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa Sekta ya Madini.
Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi- Madini, Lokeris Peter, Waziri wa Nchi- Mambo ya Ndani, Obiga Kania, Waziri wa Nchi- Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala, Namugwanya Bugembe na Waziri wa Nchi- Masuala ya Uchumi, Dkt. Kasirivu Atwooki.
Waziri Kairuki amekutana na ujumbe huo Novemba 28, 2017 katika Ofisi za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za Madini nchini ikiwemo suala la Sera, Sheria na Kanuni za Madini pamoja na masuala yanayohusu Wachimbaji Wadogo wa madini.
Majadiliano baina ya Wizara na Ujumbe huo vilevile yalihusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa Kamishna wa Madini, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Ujumbe huo utatembelea migodi mbalimbali ya Dhahabu inayomilikiwa na wazawa iliyoko mkoani Geita ili kujionea uendeshaji wa migodi hiyo na hivyo kupata uzoefu wa namna ya uendeshaji wake.
Aidha, ujumbe huo wa Mawaziri kutoka nchini Uganda, utatembelea nchi mbalimbali Barani Afrika ili kupata uzoefu wa usimamizi wa Sekta ya Madini hususan suala la Wachimbaji Wadogo.
Comments