SERIKALI imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini
kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na
wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kupata
masoko ya uhakika ya zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo (Alhamisi, Novemba 8, 2018) na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha
Nachuma katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini
Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu bei ya korosho
ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu hadi kusababisha wakulima
kugomea baadhi ya minada, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo
linafanyiwa kazi na Serikali.
“Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua
korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa
watulivu, Serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko.
Korosho zitanunuliwa tu.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya
uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda
vya mbolea, ambapo inatoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika
viwanda vikiwemo vya pembejeo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti
Maalumu, Neema Mgaya aliyetakakujua Serikali ina mpango gani katika
kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya mbolea ili
wakulima waweze kuipata kwa gharama nafuu.
Amesema viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi
mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine
viwili kimoja kitajengwa Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa
Mtwara. Kukamilika kwa viwanda hivyo kutaongeza uzalishaji wa mbolea na
kupunguza uagizaji kutoka nje ya nchi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amefafanua kuhusu suala la wakulima wa mahindi
kukosa masoko, ambapo amesema ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi
ilishatolewa. Amesema jambo hilo lilitolewa ufafanuzi na Waziri wa
Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.
Waziri Mkuu amesema licha ya kuwepo kwa kibali cha kuuza mahindi nje ya
nchi ni lazima Serikali itambue kiasi gani kinachotolewa kwa ajili ya
kuuza nje ya nchi, hivyo muuzaji anatakiwa awasisilishe taarifa zake kwa
wakuu wa wilaya. “Tunahitaji kuwa na takwimu za mauzo na bei ili kujua
kiasi kilichouzwa pamoja na kiasi cha fedha kilichopatika.”
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu ikiwemo mbolea, Waziri
Mkuu amesema suala hilo linaratibiwa vizuri na Wizara ya Kilimo na
tayari asilimia 60 ya mahitaji ya pembejeo tayari imeshaingia nchini,
hivyo Serikali itahakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Lucia Mlowe, Mbunge
wa Viti Maalumu aliyehoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu tatizo kubwa
la wakulima wa mahindi kukosa masoko ya uhakika.
Comments