Mtangazaji mkongwe wa Star TV na Radio Free Africa za Mwanza, Samadu Hassan, amefariki dunia mjini humo.
Hassan aliyewahi kufanya kazi Kenya na kupata umaarufu mkubwa atakumbukwa kwa uchapaji kazi na sauti maridadi ya utangazaji.
Akizungumza na Mwananchi Digital asubuhi hii, mdogo wa Samadu, Latifa Hassan amesema kaka yake alikuwa akisumbuliwa na kifua kwa zaidi ya wiki moja, kabla ya kufikwa na umauti usiku.
“Samadu alirudi nyumbani kwake jana jioni, akitokea kazini na alikuwa mzima wa afya, japo alikuwa akilalamika kuwa kifua kilikuwa kinamsumbua kwa takriban wiki nzima sasa,” amesema Latifa.
“Tulikuwa na maongezi naye kwa muda na baadaye tukala naye chakula hadi tukamaliza, akatueleza kifua kinamsumbua, tukamshauri pengine twende hospitali usiku huo kupata matibabu akasema angeenda kesho (leo).”
Hata hivyo anasema ilipofika saa sita kasoro usiku, ghafla hali yake ilianza kubadilika na alianguka chini na kuanza kutokwa na mapovu mdomoni.
“Hali hiyo ilitufanya tukimbie kwenda kutafuta gari ili kumuwahisha hospitali, lakini hadi tumepata gari na kurudi ndani tukakuta tayari ameshafariki,” amesema Latifa.
Tunatoa pole kwa familia yake, mwajiri wake Sahara Media na waliokuwa wafanyakazi wenzake.
Comments