Chama Cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda Na Kilimo TCCIA kimesema kinaunga mkono hatua ya Serikali ya kuamua kubangua korosho ndani ya nchi kabla ya kuisafirisha nje.
Hayo yamesemwa na kaimu rais wa chama hicho Octavia Mshiu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TCCIA.
Aidha ameongeza kuwa chama hicho kitaendelea kuishawishi sekta binafsi kuanzisha viwanda vya ubanguaji na uongezaji thamani wa bidhaa hiyo ili Tanzania ifaidike na mali ghafi nyingine zitokanazo na korosho
Sanjari na hayo amesema kuwa maadhimisho ya miaka 30 ya chama hicho yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo maonyesho ya wafanyabiashara wadogo,wakati na wakubwa wa bidhaa za ndani yatakayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja kuanzia Novemba 15, mwaka huu yenye lengo la kutangaza na kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kuziuza kwa wingi nje ya nchi ili kuimarisha uchumi wa taifa kupitia fedha za kigeni
Mbali na maonyesho hayo pia watatoa tuzo kwa kwa kampuni iliyouza bidhaa nyingi za kitanzania nje ya nchi pamoja na mdahalo ambao utashirikisha TCCI na taasisi ya Sekta Binafsi TPSF ambao utazungumzia mchango wa sekta binafsi kwenye uchumi wa nchi kuanzia ilipotoka hadi sasa.
Chama cha wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo TCCIA kilianzishwa mwaka 1988 ikiwa ni kutokana na mabadiliko ya kiuchumi ya kipindi hicho ambapo Tanzania ilijiondoa kwenye uchumi wa dola na soko hivyo Rais wa kipindi hicho Ally Hassan Mwinyi kuamua kuundwa kwa chombo hicho.
Comments