Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa
kuongeza vyanzo vya mapato kuliko kutegemea vyanzo vilivyopo.
Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Dk.Ashatu Kijaji alipokuwa akihutubia wahitimu na wageni
waalikwa kwenye mahafali ya 11 ya Chuo cha Kodi (ITA) yaliyofanyika mwishoni
mwa wiki katika viunga vya Chuo hicho kilichopo Mwenge Dar es Salaam.
Dk.Ashatu alisema kuwa TRA hawana budi kuwa wabunifu katika
kubuni miradi itakayoongeza mapato serikalini nakuepukana na lawama za
ubadhirifu kwa baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.
Vilele Dk.Ashatu alitoa miezi sita kwa mamlaka hiyo
kuhakikisha kodi ya pango la nyumba inalipwa lakini akionya kutenda haki katika
ukadiriaji wa kodi hizo kulingana na uwiano wa nyumba husika.
“Niwape miezi sita kuhakikisha Kodi ya majengo inakusanywa lakini
mtende haki kwa wananchi kwakukadiria kodi kulingana na ukubwa wanyumba, eneo
nyumba ilipo na thamani ya nyumba kwakufanya hivyo mtakuwa mmejitoa katika
lawama na mapato mtakusanya,”amesema.
Aidha Dk.Kijaji alipokuwa akijibu changamoto zilizoainishwa
na Kamishina Mkuu wa TRA Charles Kichere ambapo kubwa ilikuwa ufinyu wa bajeti ambayo TRA na Chuo cha Kodi
wanapatiwa na Serikali, Dk. Ashatu aliwataka wabuni miradi endelevu ambayo
itawapatia fedha nakuweza kuendesha majukumu yao ya kiutendaji.
“Kwa TRA niwaombe mbuni miradi endelevu itakayo wasaidia
katika kukabiliana na kampeni na doria kwa wakwepa kodi kwakufanya hivyo
mtakuwa mmefanikiwa lakini pasipo kufanya hivyo suala la kukusanya kodi
kwakutegemea bajeti yenu ni gumu,”amesema.
Kwa upande wa Chuo cha Kodi Dk. Ashatu alipokuwa akijibu
changamoto zilizo ainishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Dk. Samwel Werema,
kuhusu ufinyu wa bajeti wa Chuo hicho, Dk Ashatu alikitaka chuo kuandika
maandiko na kufanya tafiti zitakazo waongezea fedha kwa ajili yakuendesha Chuo.
Mkuu wa Chuo Profesa Isaya Jairo aliiomba Serikali kuongeza
bajeti ya uendeshaji wa chuo ili kuzalisha wataalamu bora zaidi hususani wale
wanaobaki kufundisha ili wapatiwe mafunzo zaidi nje ya nchi ili warudipo watoe
mchango mkubwa katika chuo na Taifa.
Hata hivyo wahitimu waliaswa kujiepusha na tamaa ya utajiri
wa haraka ambao utawaingiza katika rushwa ambapo watakapo bainika watakosa
ajira na kunyang’anywa cheti.
“Jiepusheni
na rushwa, rushwa ni adui wa haki na maendeleo ,msitafute utajiri wa haraka
Taifa linawategemea mkawe hodari na waaminifu huko makazini mkaoneshe utofauti
na wahitimu wengine ili tujivunie kuwa tumezalisha wahitimu bora,”amesema.
Comments