KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva usiku wa jana ameifungia klabu yake, Difaa Hassan El- Jadidi katika sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji, Rapide Oued Zem kwenye mchezo wa wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola Pro Uwanja wa Maniapaa ya Oued Zem.
Msuva, mchezaji wa zamani wa Yanga SC aliye katika msimu wake wa pili Jadidi, alifunga bao lake dakika ya 31, kabla ya Issam Boudali kuisawazishia Rapide Oued Zem dakika ya 90 na ushei.
Kwa matokeo hayo, Jadida inafikisha kwa pointi 10 baada ya kucheza mechi saba, ikiendelea kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ya Morocco – na wapinzani wao, Rapide Oued Zem wanabaki nafasi ya sita kwa pointi zao 11 pia, ingawa wao wamecheza mechi nane sasa.
Simon Msuva akikimbilia mpira jana Uwanja wa Maniapaa ya Oued Zem
Simon Msuva (katikati) katika mchezo wa jana dhidi ya Rapide Oued Zem
Simon Msuva katika kikosi cha Difaa Hassan El- Jadidi kilichoanza jana
Hassania Agadir ndiyo inaongoza Ligi Kuu ya Morocco kwa pointi zake 14 sawa na Youssoufia Berrechid, wakifuatiwa na Olympic Safi yenye pointi 12 wote wakiwa wamecheza mechi nane.
Mabingwa wawili wa zamani Afrika na mahasimu wa jiji la Casablanca, Raja Casablanca wapo nafasi ya 11 kwa pointi zao tisa za mechi tano na Wydad Casablanca wanashika mkia kwa pointi zao sita za mechi nne.
Comments