HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA MHE. GEORGE H. MKUCHIKA (MB), KWENYE UFUNGUZI WA KONGAMANO KUHUSU “KUKUZA NA KUIMARISHA UONGOZI NA VIONGOZI TANZANIA”, KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA KIMATAIFA WA MWALIMU JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM, 02 NOVEMBA, 2018
MHESHIMIWA MIZENGO PINDA, WAZIRI MKUU MSTAAFU WA JAMUHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA,MHESHIMIWA ANNE MAKINDA, SPIKA MSTAAFU WA JAMUHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,DKT. LAUREAN NDUMBARO, KATIBU MKUU, OFISI YA RAIS -MENEJIMENTI YA
UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA,PROF. JOSEPH SEMBOJA, AFISA MTENDAJI MKUU, TAASISI YA UONGOZI,VIONGOZI WASTAAFUVIONGOZI WA VYAMA
VYA SIASA, SERIKALI, MASHIRIKA YA UMMA, BINAFSI NA ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI,WAGENI WAALIKWA,WAANDISHI WA
HABARI,MABIBI NA MABWANA.
Napenda nitumie
fursa hii kuwashukuru waandaaji wa Kongamano hili, Taasisi ya UONGOZI, kwa
kunipa heshima kubwa ya kuwa Mgeni Rasmi. Nawashukuru na kuwapongeza kwa
maandalizi mazuri ya Kongamano hili lenye umuhimu mkubwa, hasa wakati huu
ambapo Serikali inakamilisha matengenezo ya Program ya Maboresho ya Utumishi wa
Umma Awamu ya Tatu ambayo inatambua na kusisitiza umuhimu wa kukuza na
kuimarisha Uongozi na viongozi ndani ya Sekta na Umma. Hivyo, mawazo
yatakayotokana na mjadala wa leo yatatumika kuimarisha Program hii ya maboresho
Serikalini.
Ndugu Washiriki;
Kongamano hili
kuhusu “Kukuza na Kuimarisha Uongozi na
Viongozi Tanzania” ni muhimu kwetu sote; Serikali, Bunge na Mahakama; Mashirika
ya Umma na Binafsi na; Vyama vya Siasa na Asasi zisizo za Kiserikali. Litatoa
fursa ya kubadilishana taarifa, mawazo na uzoefu kuhusu dhana ya uongozi na mikakati
ya kukuza na kuimarisha uongozi na viongozi nchini Tanzania na kwingineko. Litatoa fursa ya kutathmini hali ilivyokuwa huko
nyuma, tangu miaka ya uhuru, hadi hivi sasa; na yapi mazuri yakuendeleza huko
tuendako.
Uongozi
bora ni msingi wa maendeleo endelevu katika jamii au taifa lolote duniani. Baba
wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliliona hili na kuliweka
wazi alipotamka masharti manne ya maendeleo kwa Taifa ambayo ni: watu, ardhi,
siasa safi na uongozi bora. Hili la uongozi bora ambalo ndio mada yetu ya leo
alilifanyia kazi kwa nguvu zake zote.
Ndugu Washiriki;
Kuandaa,
kujenga na kuimarisha uongozi na viongozi wa sasa na wa baadaye ni mchakato mpana
unaohusisha mifumo rasmi na isiyo rasmi. Kwa Tanzania, ni mchakato ulioanza
kabla ya uhuru wa Tanganyika, ambapo Chama cha TANU katika miaka ya mwisho ya
1950 kiliamua kuanzisha Chuo cha Kivukoni kwa lengo la kuandaa viongozi wa ngazi
za juu katika Taifa jipya la Tanganyika. Aidha, Taasisi ya Mzumbe (Institute of
Development Management) ililenga kujenga viongozi wa Serikali za Mitaa hadi
mwanzoni mwa miaka ya 1970 ambapo Serikali za Mitaa ziliondolewa. Baada ya hapo
IDM ilijikita kujenga viongozi katika utumishi wa Umma.
Kabla ya miaka ya
mwanzoni ya 1980, dhana ya uongozi ilijengwa ndani ya misingi ya itikadi ya Siasa
ya Ujamaa na Kujitegemea. Mihimili yote mitatu ya Dola ilielekeza nguvu zake katika
kujenga uongozi na viongozi watakaoifikisha jamii katika ndoto ya Ujamaa na
Kujitegemea. Mifumo na taasisi zilianzishwa kukidhi matakwa haya. Kwa mfano, Chuo
cha Kivukoni kilibadilika na kuwa Chuo cha Itikadi ya Chama Tawala cha TANU na
baadaye CCM ya Ujamaa na Kujitegemea; mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (National
Service) yalianzishwa kwa lengo la kujenga umoja na usawa kati ya jamii ya
vijana Wa-Tanzania; Sekretarieti ya
Maadili (Ethics Secretariat) ilianzishwa kwa lengo la kujenga uadilifu na
maadili mema katika Utumishi wa Umma na; Taasisi ya Kuzuia Rushwa
(Anti-Corruption Squard) ilianzishwa ili kutiisha uaminifu kwa wananchi wote. Aidha,
mifumo ya ajira, malipo na maendeleo ya Watumishi wa Umma, ilijengwa ndani ya
itikadi ya Chama Tawala ya Ujamaa na Kujitegemea.
Mchakato wa kujenga
uongozi na viongozi ulihusisha pia sekta binafsi na asasi zisizokuwa za umma, kama
vile za kidini, tasnia ya burudani kama vile muziki na maonyesho, familia na
jamii yote kwa ujumla. Kila mmoja kwa nafasi yake alishiriki katika kujenga uongozi
na viongozi wenye mrengo wa kijamaa na kujitegemea.
Ndugu Washiriki;
Mabadiliko ya
kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyofanyika katikati ya miaka ya 1980 yalileta athari
kubwa kwenye mifumo ya kujenga uongozi na viongozi wa Taifa letu. Tafsiri ya
Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ilibadilika, kutokana na kuanzishwa kwa mfumo
wa vyama vingi vya siasa, na uchumi wa soko huria. Kwa bahati mbaya, swala la uongozi
na namna gani viongozi waandaliwe kuongoza mabadiliko haya ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii haikupewa kipaumbele kama ilivyokuwa hapo awali. Aidha, mifumo na
taasisi zilizokuwa zikiandaa viongozi zilibadilisha malengo na muelekeo wake.
Kwa mfano, Taasisi ya IDM Mzumbe ilibadilishwa na kuwa Chuo Kikuu. Chuo cha Kivukoni kiliporomoka na baadae kikabadilishwa
na kuwa Chuo Kikuu, na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (national service) yalisitishwa.
Taasisi za sanaa
kama vile za burudani, muziki na maonyesho zilibadilisha muelekeo; ziliacha ajenda
ya kuandaa uongozi na viongozi wenye kubeba ajenda ya kitaifa. (Inawezekana pia
hawakujua ajenda ya kitaifa ni ipi). Familia na jamii kwa ujumla zilijielekeza
kuiga maisha na utamaduni wa nchi za magharibi. Hadi mwanzoni mwa miaka ya 2010
hakukuwepo na mfumo na taasisi iliyokuwa na ajenda bayana ya kuandaa uongozi na
viongozi wa Tanzania tunayoitaka. Hali hii ilisababisha ombwe katika uandaaji
wa uongozi na viongozi na hivyo kuhatarisha kufikia matarajio ya Taifa.
Ndugu Washiriki;
Serikali ililiona
hili tatizo, na kuanzia mwaka 2010 ilianza kuchukua hatua madhubuti za
kuendeleza uongozi na viongozi nchini. Taasisi ya UONGOZI ilianzishwa mwaka
2010 ikiwa na lengo la kuwajengea viongozi wa Kiafrika uwezo wa kufikia
maendeleo endelevu kwa wananchi wake; Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence
College) kilianzishwa mwaka 2012 kwa ajili ya kuwaandaa maafisa wa ngazi za juu
Serikalini kushika majukumu ya kiuongozi ya kimkakati; mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
yamerejeshwa kwa lengo la kujenga umoja, mshikamano na usawa miongoni mwa vijana
wetu; taasisi za kujenga maadili ya uongozi na viongozi zimeimarishwa; n. k.
Ndugu Washiriki;
Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria
kwa dhati kuandaa na kuendeleza uongozi na viongozi nchini. Mifano michache
inathibitisha dhamira hiyo. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais ametangaza kuanzishwa
Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kinacholenga kujenga
uongozi na viongozi katika nchi zilizokuwa za mstari wa mbele
katika ukombozi wa Bara la Afrika. Zaidi ya hayo, Serikali imeendelea kuimarisha
nidhamu katika utendaji wa kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma,
kujenga jamii yenye uadilifu na inayochukia rushwa. Aidha, Serikali
imetengeneza Programu ya Maboresho Awamu ya Tatu ambayo sehemu kubwa inalenga
kujenga mfumo wa kuandaa viongozi Serikalini. Jitihada hizi ni muhimu sana
katika kuendeleza uongozi na viongozi wenye sifa chanya na zinahitaji kuungwa
mkono na sisi sote.
Ndugu Washiriki;
Kwa kumalizia,
napenda niwapongeze tena wote kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye kongamano hili
muhimu lenye lengo la kujadili namna gani tunaweza tukajenga na kuendeleza
uongozi na viongozi nchini. Uwepo wenu hapa unadhihirisha dhamira yenu katika
kuisaidia Serikali kufikia lengo hili muhimu.
Aidha, ni matarajio
yangu kuwa baada ya kongamano mtaweza kuibua mambo muhimu yatakayoiwezesha
Serikali kuandaa na kujenga uongozi na viongozi wenye sifa za kuongoza jamii ya
Watanzania ya hivi sasa na hata ile ya wakati ujao. Swali la msingi kwa washiriki
wa kongamano ni: Je, ni mfumo upi na mkakati gani utaliwezesha Taifa kuandaa na
kujenga uongozi na viongozi wa Taifa letu; kwa kuzingatia mazingira na mahitaji
yetu, ya kanda na ya kimataifa?
Ndugu Washiriki;
Baada ya kusema
haya, naomba sasa kutamka kuwa Kongamano hili limefunguliwa rasmi, na nawatakia
ushiriki mwema.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Comments