NYOTA wa zamani wa Simba wameipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini wameishauri Kamati ya Usajili ya timu hiyo kusaka washambuliaji wapya watakaowaongezea nguvu Emmanuel Okwi na John Bocco.
Aliyekuwa nahodha wa timu hiyo na sasa ameajiriwa na Mtibwa Sugar, Hassan Isihaka, alisema Okwi na Bocco wamefanya kazi nzuri, lakini wanatakiwa kutafutiwa washindani wao.
“Okwi na Bocco wakiwa na washindani pia itawasaidia wasibweteke bali wataongeza juhudi ya kugombania namba na hata ikitokea wakaumia pengo lao litazibwa,” alisema.
Danny Mrwanda aliyeichezea Simba kwa nyakati tofauti, alisema washambuliaji wa timu hiyo wanapaswa kuwa wengi na wakali kama walivyo nyota wa safu ya kiungo kikosini humo.
Aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Masoud Nassor ‘Chollo’ alisema kuelekea michuano ya kimataifa, Simba inatakiwa kusajili washambuliaji makini zaidi.
“Watafute wakali kuliko Okwi na Bocco. Wachezaji watakaokuwa chachu ya kikosi kupata matokeo wakati wote,” alisema.
Comments