Mtendaji wa Kata ya Mwadui iliyopo mwambao wa Bonde la Ziwa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga, Benedict Chapewa ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Kamanda wa polisi Mkoani humo George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo, na kwamba Chapewa ambaye aliwahi kuwa katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sumbawanga, alivamiwa na kundi la watu wasiojulikana wakati akiwa anakunywa pombe katika moja ya baa anayomiliki kijijini hapo.
Kamanda Kyando amesema kuwa Watu hao walimmiminia risasi kwa kutumia bunduki aina ya gobore kisha kumkata kata na mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Aidha, amesema uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo unaendelea kufanyika na watuhumiwa wanasakwa popote walipo ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Pia ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni ukiukaji wa haki za binadamu na vyombo vya dola vitahakikisha vinawachukulia hatua za kisheria wale wote wanajichukulia sheria mkononi.http://mjengwablog.com
Comments