Kocha Mfaransa Pierre Lechantre, amepanga kufumua kikosi chake na
kukisuka upya kwa mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya
kimataifa.
Katika mkakati huo, Lechantre anatarajia kuwatema wachezaji zaidi ya saba ili kutoa nafasi kwa wapya kusajiliwa.
Simba inatarajiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
Hata hivyo, Lechantre atakuwa na uhakika wa kutimiza ndoto yake endapo klabu ya Simba itamuongeza mkataba mpya.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema mkataba wa
Lechantre unatarajiwa kujadiliwa na Kamati ya Utendaji baada ya
kumalizika mechi za Ligi Kuu Jumatatu wiki ijayo.
Akizungumza jana, Lechantre alisema anataka kuisuka Simba iwe na nguvu
ya kushindana na miamba mingine ya soka Afrika katika mashindano ya
kimataifa, hivyo atalazimika kuwatema baadhi ya wachezaji maarufu.
Panga la wachezaji saba linatarajia kuwapitia Juuko Murshid, Laudit
Mavugo, Juma Liuzio, Jamal Mwambeleko, Mwinyi Kazimoto, Mohammed Ibrahim
na Nicholas Gyan.
Kazimoto, Mavugo na Ibrahim mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu
huu na uwezekano wa kuongezwa ni mdogo wakati Gyan licha ya kucheza mara
kwa mara anatarajiwa kutolewa kwa mkopo.
Lechantre alisema baadhi ya wachezaji hakuridhika na viwango vyao tangu
alipoanza kazi Simba na ametoa baraka kutolewa kwa mkopo au kuachwa.
“Wachezaji wote ni wazuri lakini uwezo wao unazidiana, kuna baadhi ambao
nitawaambia kama wamepata timu za kucheza ruksa kuondoka, wameshindwa
kupata nafasi na viwango vyao vitapotea,” alisema Lechantre.
Lechantre alisema anataka washambuliaji wawili, beki wa kati na kulia,
kiungo mkabaji na winga mmoja ambao watakuwa na tija katika program
yake.
“Mkakati wangu kuwa na wachezaji 11 bora ambao wataanza katika kikosi
cha kwanza, pia nataka watakaokuwa benchi wawe na uwezo kama walioanza
kikosi cha kwanza,” alisema Lechantre.
Gharama
Msimu huu Simba ilitumia Sh1.3 bilioni katika usajili wa wachezaji 14,
ambao ni Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Shomari Kapombe,
Erasto Nyoni, John Bocco, Yusuph Mlipili, Salum Mbonde, Said Mohammed,
Emmanuel Mseja, Ally Shomari, Jamal Mwambeleko, Poul Bukaba na Nicholas
Gyan.
Thamani ya usajili iliongezeka katika dirisha dogo, baada ya kumpata
beki Mghana Asante Kwasi kutoka Lipuli na kwa ujumla wao ndio walioipa
ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Comments