MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey
Mwambe amefanya ziara ya kikazi nchini Ujerumani na Uholanzi kati ya
Mei 14 na 17 mwaka huu katika jitihada zake za kutangaza fursa
za uwekezaji ili kushawishi na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania
Bw. Geoffrey Mwambe (kulia) alipomtembelea Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mhe. Dkt.
Possi Abdallah ofisini kwake Berlin, Ujeruman
Akiwa nchini Ujerumani Bw. Mwambe alisema lipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini
Ujerumani Mhe. Dkt. Possi Abdallah ambapo walifanya kikao cha kazi kabla
ya kushiriki kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Ujerumani na nchi
za Afrika Mashariki lililofanyika Mei 15, 2018 katika mji wa Berlin.
Pichani baada ya kukamilisha zoezi la kusaini MOC . waliokaa kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe na kushoto ni Mwenyekiti wa DCIB Bw. Hans Biesheuvel. Pamoja nao kulia ni Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa TIC Bw. John Mnali,Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe. Irene Kasyanju,Mkurugenzi Mkuu wa DCIB Dkt Dewanand Mahadew na Bi Zeinab Dauda Meneja wa DCIB Afrika Mashariki.
Alisema Kongamano hilo liliandaliwa ili kutoa nafasi kwa nchi za ukanda wa Afrika
Mashariki kunadi fursa za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Ujerumani
na dunia kwa ujumla.
Vilevile siku mbili baada ya kongamano, Kituo kilifanya ziara nchini Uholanzi ambapo kilifanikiwa kusaini makubaliano ya mashirikiano (MOC) na Taasisi ya
Biashara za Kimataifa ya Uholanzi (DCIB) pamoja na kufanya mkutano na baadhi
ya wafanyabiashara wa Taifa hilo wenye nia ya kuja kuwekeza nchini.
Sekta zitakazohusika ni pamoja na mafuta, gesi, kilimo, afya, usafirishaji,
viwanda, fedha, mazingira, nishati na mawasiliano.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe alipomtembelea Balozi wa Tanzania nchini
Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju ofisini ,The Hague, Uholanzi.
"Kupitia kongamano hilo niliwezakuelezea majukumu ya Kituo,msaada unaotolewa
kwa wawekezaji katika kuanzisha miradi, hali ya uchumi na mikakati mbalimbali
inavyotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa lengo la kuboresha mazingira
ya biashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa mitaji ya kutoka nje (FDI),
"alisema Bw. Mwambe.
Akiainisha baadhi ya maeneo ambayo yanafanyiwa kazi na Serikali alisema kuwa ni
pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya usajili wa biashara na leseni kwa wawekezaji
wa ndani na nje pamoja na kuondoa urasimu ndani ya mifumo ya Serikali kuanzia ngazi
ya Mtaa/Kijiji hadi Taifa ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji kwa
muda mfupi.
Bw. Mwambe alisema pia aliwahakikishia wawekezaji wa nchini Ujerumani na Dunia kwa ujumla
kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi na mahali salama kwa uwekezaji ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika; hivyo wawekezaji wenye mitaji na teknolojia
wanakaribishwa kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ambazo kwa sasa ni kipaumbele
cha Taifa yaani viwanda, kilimo, madini, mifugo, uvuvi, miundombinu,
uzalishaji na usambazaji umeme na miundombinu kwa ujumla.
Nae mwakilishi wa Benki ya Stanbic kwa Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Jibran
Qureishi alieleza kuwa kwa sasa Tanzania inafanya vizuri katika masuala ya
Kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Matokeo
hayo chanya ni kutokana na uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe
Magufuli aliyeanzisha vita ya kupambana na rushwa; na kupunguza
urasimu kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Bw. Qureishi ambaye ni mchumi mbobezi aliweka bayana kwamba Tanzania ina
nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi katika nyanja ya uchumi kwa
miaka ya hivi karibuni baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya maendeleo
inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia rasilimali za ndani na sio mikopo
kama ilivyokuwa imezoeleka.
Akitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler's
Gorge, ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma na upanuzi
wa bandari. Kwa ujumla ziara ya Kituo nchini Ujerumani na Uholanzi
imekuwa ya manufaa yenye manufaa .
"kwa upande wa Ujerumani tumekutana na makampuni ambayo yameonesha nia ya
kuwekeza kwenye sekta za viwanda, afya, ujenzi, miundombinu, mawasiliano,
usafirishaji na nishati,pili kuanza kwa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano
kati ya Kituo na Taasisi ya Biashara za Kimataifa ya Uholanzi kunatoa fursa ya
kutekelezwa masuala mbalimbali kwenye miradi ya ubia, upatikanaji wa fedha za
miradi, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, kuandaa semina au warsha na misafara
ya wawekezaji,"alisema Bw. Qureishi.
Alisema pia kituo kinatarajia kupokea kundi la kwanza la wafanyabiashara
kutoka Uholanzi mapema mwaka 2018 hadi 2019 na jambo la tatu kwa upande wa
Uholanzi wamekutana na makampuni yaliyoonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta
za utalii, ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza spea za magari, uanzishaji wa
chuo cha mafunzo ya ufundi (Vocational Training), uanzishaji wa mradi wa
usimamizi wa usalama wa mizigo kuanzia bandarini mpaka eneo husika na usimikaji
wa mitambo ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngano.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju amesema
kusainiwa kwa makubaliano kati ya TIC na DCIB ni hatua kubwa ambayo itarahisisha
utekelezaji wa sera, diplomasia ya uchumi. Mhe. Balozi amehitimisha kwa kuhimiza
wadau wa sekta binafsi ya Tanzania kutumia vema makubaliano hayo kama fursa ya
kuongeza biashara na uwekezaji kwa kushirikiana na wadau kutoka Uholanzi.
Comments