Simba inahitaji pointi tano tu kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu na kiungo
wao Mnyarwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas' aliyekosa mechi dhidi ya
Yanga, amerudi kuungana na wenzake na kupigania ubingwa huo waliukosa
kwa takribani miaka mitano.
Niyonzima amerudi akitokea kwao Rwanda alipokuwa kwenye msiba wa dada
yake anayeitwa Sumaye jambo lililomsababishia akakosa mchezo dhidi ya
Yanga mwishoni mwa mwezi uliopita.
Amerudi na kukuta timu yake inahaha kusaka pointi tano ambazo
zitawatangaza kuwa mabingwa msimu huu na hiyo ni baada ya kucheza mechi
26 na kuvuna pointi 62 sasa wanahitaji hizo tano ili wafikishe 67 ambazo
hazitafikiwa na timu nyingine yeyote.
Yanga ndiyo timu pekee wenye nafasi ya kuwapindua Simba kama watapoteza
mechi zao baada ya kucheza mechi 24 na kufikisha pointi 49, wakishinda
mechi zao zote sita zilizobaki watakuwa na 66 na ndiyo nafasi yao pekee.
Kwani Azam inayowafuata nyuma, wao wameshautema rasmi ubingwa huo kwa
sababu mechi 26 walizocheza wamepata pointi 49, hata wakishinda zote
nne zilizobaki watakuwa na 61 tu.
Meneja wa Simba, Richard Robert amesema: "Haruna amesharudi na kuungana
na wenzake kwenye timu kwa ajili ya maandalizi ya michezo mingine ijayo.
Ameshaanza mazoezi na wenzake na kila kitu kinakwenda sawa."
Comments