Skip to main content

Paul Makonda waliokabidhiwa miradi ya ujenzi kuzitendeahaki fedha za kodi za wananchi



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka Wakandarasi wote waliokabidhiwa miradi ya ujenzi wa barabara kuhakikisha wanazitengeza barabara kwa kiwango kinachotakiwa  na kwamba watakaofanya chini ya kiwango watazirudia kwa gharama zao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Akizungumza Dar es Salaam jana katika wa Hafla fupi ya kusainisha mikataba minane ya ujenzi wa miradi ya barabara  iliyojumisha Ofisi ya mkoa huo, Wakala wa Barabara za  Vijijini na Mijini-Tanzania (TARURA) na wakandarasi mbalimbali Paul Makonda  ameitaka TARURA kuhakikisha ndani ya wiki mbili barabara zote zilizojengwa chini ya kiwango zinarudiwa.
Alisema wakandarasi wanaokabidhiwa miradi ya barabara wamekuwa na tabia ya  kutotekeleza majukumu yao ipasavyo kwani barabara wanazozijenga huharibika ndani ya muda mfupi na kusababisha adha kwa watumiaji.
“ Nitoe rai kwa wakandarasi watakaoshindwa kuzitendea haki fedha za kodi za wananchi kwa kujenga barabara chini ya kiwango watazigharamia wenyewe,” Alisema Makonda.
Amebainisha kuwa wakandarasi wanatakiwa kuacha tabia ya kutoa rushwa wakati wakidai malipo na kwamba wawasiliane na mamlaka husika walipe stahiki zao.
Amewahimiza watendaji kutenga muda wa kwenda kuangalia maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara zitakazojengwa na zinazoendelea kujengwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi ya Zabuni ya Tarura mkoani humo, Devota Ndusilo ameitaja miongoni mwa  miradi ya ujenzi huo ni barabara ya Tegeta-Nyuki, Msasani-Mikocheni, Haile Sellasie na Sea Clif- Mikocheni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KGG Investment Ltd, Richard Mlay amesema ana imani wakandarasi wote watazitendea haki barabara walizokabidhiwa kwa kiwango cha juu.



Comments