Wizara ya Fedha na Mipango Fungu Hamsini (Vote 50)linalohusika na masuala ya utawala, limeibuka kinara kwa kupata tuzo ya mshindi wa kwanza katika utoaji wa Taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 katika kundi la Wizara na Idara za Serikali inayoandaliwa na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA).
Tuzo hizo zimetolewa kwa washindi na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Francis Mwakapalila kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa Mkutano wa mwaka wa Wahasibu nchini uliofanyika katika eneo hilo.
CPA. Mwakapalila alisema kuwa taarifa bora za fedha ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi kwa kuwa walipa kodi, wawekezaji na wadau wengine hutegemea taarifa hizo katika kufanya maamuzi.
‘Kama taarifa za fedha hazitatolewa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati mwafaka kunaweza kusababisha athari katika uthabiti wa mifumo ya kifedha nchini’, alieleza CPA. Mwakapalila
Aidha Mwakapalila amewapongeza wahasibu kwa kuamua kukaa pamoja na kujadili taaluma ya uhasibu katika maendeleo ya viwanda ambayo ni ajenda ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya tano.
Amesema suala la Uchumi wa viwanda ni muhimu katika kuongeza kipato na kupata fedha za kigeni kwa njia ya kuuza bidhaa nje na pia kupata mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hivyo akatoa rai kwa wananchi kuendelea kujadili masuala ya uchumi wa viwanda na kupata namna sahihi ya kuufikia ili ndoto ya uchumi huo ziweze kuwa za kweli.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), CPA. Pius Maneno amesema kuwa tuzo zinazotolewa na NBAA zinalengo la kuhamasisha uwajibikaji na kuandaa taarifa ya fedha zilizo na viwango vya kimataifa.
Amesema kuwa washindi wa tuzo hizo wanapatikana kupitia mchakato uliosheheni weledi wa hali ya juu kutoka kwa wabobezi wa taaluma ya uhasibu nchini ambao wanaangalia vigezo kadhaa vikiwemo kuwa na hati safi na kuwasilisha Hesabu kwa wakati na pia kufikisha kiwango cha ubora wa taarifa kuanzia asilimia 75.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Fungu 50, Bw. Christopher Nkupama, amesema kuwa tuzo hiyo inawapa morali ya kufanyakazi kwa umahili zaidi na kuwapongeza watumishi walioko katika idara yake kwa kufanyakazi kubwa na bila kuchoka kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni na taratibu za uhasibu wanapotekeleza majukumu yao.
Mshindi wa Jumla katika tuzo hizo kwa taarifa bora ya fedha kwa mwaka 2016 ni Twiga Cement Plc na kwa upande wa Wizara na Idara za Serikali ni Wizara ya Fedha na Mipango fungu hamsini (V. 50), tuzo ambayo ilipokelewa na Mhasibu Mkuu wa fungu hilo Bw. Christopher Nkupama, ikifuatiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji fungu arobaini na nne (V.44) na Ofisi ya Waziri Mkuu fungu ishirini na tano (V. 25)
Washiriki wa Tuzo hizo ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakala wa Serikali, Wizara na Idara za Serikali na Sekta Binafsi ambapo kwa mwaka huu waliojitokeza kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa walikua sita na Wizara na Idara za Serikali walikua sita.
Jumla ya washidani waliojitokeza ni 56 na waliofanikiwa kuvuka kigezo cha kuwa na zaidi ya asilimia 75 walikua washidi 36 na hao walifanikiwa kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu kulingana na makundi.
Vilevile Idadi ya Wahasibu ambao wamehudhuria katika Mkutano wa mwaka ambao hufanyika kila mwaka kabla ya kutolewa tuzo hizo imepanda kwa asilimia 60 ambapo mwaka 2016 walihudhuria wajumbe 1700 ilihali mwaka huu 2017 wamehudhuria zaidi ya wajumbe 2700
Comments