WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan pindi atakapohamia Dodoma.
Waziri Mkuu amefanya ukaguzi huo leo mchana (Jumatano, Desemba 6, 2017) katika eneo la Kilimani, mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Waziri wa Nchi (OWM) anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Wenye Ulemavu na Vijana, Bibi Jenista Mhagama alisema Kikosi kazi cha kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kilibaini kuwa mahali alipokuwa akiishi awali siyo sahihi kwa ajili ya makazi ya kudumu ya Mhe. Makamu wa Rais.
“Pale palikuwa panafaa kwa ajili ya ziara za kikazi alipokuwa akija Dodoma, kwa hiyo tumeamua tufanye ukarabati hapa, ili aweze kuishi kwa viwango vinavyostahili.”
Alisema kazi ya matengenezo kwenye makazi yake itagharimu sh. bilioni 1.5 wakati kazi ya kutenganisha ofisi za watumishi na wasaidizi wa Makamu wa Rais itagharimu sh. milioni 680.
Waziri Mkuu pia alikagua matengenezo ya Ofisi inayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais ambayo itakuwa eneo la Ndejengwa.
Wakati huohuo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Bw. Steven Simba ambaye anasimamia ujenzi huo, alimweleza Waziri Mkuu wanataraji kuwa kazi hiyo itakamilika kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.
Comments