Na mwandishi wetu
CHAMA cha Mapinduzi(CCM) kimedai kuwa baadhi ya wabunge wa Chadema na CUF wa majimbo ya Dar es Salaam wanataka kujiunga na chama hicho.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
CCM inatoa kauli hiyo wakati kukiwa na minon’gono kuwa viongozi waandamizi wa upinzani wanaojiunga CCM wananuliwa huku chama hicho kikikanusha na kutoa sababu kuu mbili ya kupata wanachama hao.
Wiki iliyopita chanzo kimoja kimeeleza jijini Dar es Salaam , katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema baadhi ya wabunge hao wameonesha nia ya kujiunga na chama hicho.
Bila kutaja idadi wala majina ya wabunge hao Polepole amesema “Wewe utaona ‘soon’ muda si mrefu kuna wabunge kutoka majimbo ya Dar es Salaam wa UKAWA wameonesha nia ya kutaka kujiunga CCM.’’
Kuhusu sababu za wapinzani kujiunga CCM Polepole amesema ni uongozi na utendaji mbovu wa viongozi wa kitaifa wa vyama vya upinzani ambao hauzingatii kanuni na taratibu zao
“Ukweli hawa viongozi waandamizi wa upinzani wanaojiunga CCM hatuwarubuni wala kuwapa fedha. Watu hawaelewi wala kufuatilia kwa undani, wengi wa waliojiunga CCM ukizungumza nao wanakueleza kuwa wamechoka na jinsi wanavyoongozwa na viongozi wao wa kitaifa,’’ amesema na kuongeza
“Wanasema wanaweza kufanya maamuzi fulani ndani ya chama na kwa kufuata utaratibu halali ikiwemo kuchaguana lakini mwenyekiti taifa anakuja na kutengua maamuzi hayo ‘so’ hivyo unatarajia nini kitatokea hapo. Lazima sintofahamu itajitokeza.’’
Polepole ametaja sababu nyingine ni kukubali utendaji wa rais Magufuli hasa anavyoshughulikia masuala ya ufisadi na rushwa.
“Hili la kupambana na ufisadi na rushwa wao wenyewe wanalizungumza hivyo ni mojawapo ya mambo yanayowavutia kujiunga CCM,’’ amesema
Hata hivyo kufuatia utete wa hali hiyo hii leo ofisi ya mbunge wa Temeke imekanusha vikali uvumi wa mbunge wa jimbo hilo, Abdallah Mtolea(CUF) kujiuzulu ubunge.
Katibu wa mbunge huyo, Rajab Matata amesema “Ukweli ni kwamba aliejiuzulu ubunge ni Mh. Maulid Said Abdallah Mtulia aliekuwa Mbunge Wa jimbo la Kinondoni. Na sio Abdallah Ali Mtolea Mbunge wa jimbo la Temeke. Mtolea hajajiuzulu na hana mpango Wa kujiuzuru, anawaudumia wakazi wake wa Temeke.”
Amesema wanaomuhusisha na upotoshaji huo ni watu wasio na nia njema na wenye lengo la kuwasumbua wananchi wa Temeke na watanzania.
Jana aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kinondoni(CUF) Maulid Mtulia alijiuzulu wadhifa wake huo na kujivua uanachama wa CUF pamoja na nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho na Bungeni.
Mtulia anakuwa ni mbunge wa pili katika kipindi cha takribani mwezi mmoja kujiuzulu nyadhifa hiyo baada ya aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii katika serikali ya awamu ya nne, Lazaro Nyalandu kung’atuka CCM na kujiuzulu ubunge wa Singinda Kaskazini.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments