Mbunge Viti Maalumu mkoa wa Geita kupitia Chadema, Upendo Peneza amewataka wabunge wanaotaka kujiuzulu ubunge katika kipindo hiki kuvumilia hadi mwaka 2019 ili kuliepusha Taifa kuingia gharama ya kurudia uchaguzi.
Peneza ametoa wito huo leo alipokuwa anazungumza na wanahabari ambapo amesema kama Mbunge anataka kuunga mkono Jitihada za Rais John Magufuli anaweza akafanya hivyo Bungeni hadi pale muda wake utakapoisha ndipo ang’atuke.
“Ningewaomba watusaidie kwa hii miaka 5 au wavumilie hadi mwaka 2019 sababu katiba hairuhusu kurudia uchaguzi kwa kipindi hicho, ambapo nchi haitaingia gharama za kurudia uchaguzi hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu 2020,” amesema.
Peneza amedai kusikitishwa na kujiuzulu kwa baadhi ya wabunge kwa madai kuwa sababu wanazotoa si za kweli.
” Wanaosifu kuna maendeleo watuonyeshe kazi iliyofanyika ni ipi kuliko kuuharibu upande mmoja kwa kusema kazi inafanyika wakati hali bado ni mbaya. Taifa tunaingizwa kwenye presha ya uchaguzi kabla ya 2020, wananchi wanahitaji maendeleo na mabadiliko, wananchi tuchague tunataka nini, ikiwemo kuona kodi zetu zinatumika kuleta maendeleo badala ya kutumika kwenye soko,
“Pesa zinazotumika zingesaidia kuleta maendeleo na kutoa huduma za kijamii kwenye majimbo husika. Wanaotaka kumuunga mkono rais wafanye hivyo bungeni siyo kuwaingizia watanzania gharama,” amesema.
Peneza amewataka wananchi wa majimbo husika kutowachagua wabunge waliojiuzulu endapo watataka kugombea tena, huku akidai kuwa, kama Katiba inaruhusu kungefunguliwa kesi mahakamani kuzuia wabunge hao kujiuzulu endapo uchunguzi utafanyika na kubainika kuwa sababu wanazotoa si za kweli.
“Nimejaribu kupitia katiba ili nione kama kuna kifungu kitwkachoweza kuzuia wabunge hao kutojiuzulu au chaguzi kwenye maeneo hayo kutofanyika, uchunguzi ufanyike ili kujua ukweli wa sababu zao na ikiwezekana wakitaka kugombea wasiruhusiwe, hicho kipengele sijakipata,” amesema
Comments