Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi- Idara ya Rasilimali Watu katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji Bi. Visensia Kagombora (katikati) kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu ubomoaji wa majengo ya Wizara hiyo yaliyopo katika eneo la Ubungo maji Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale. (Picha na Maelezo)
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha inamaliza changamoto ya msongamano na kuziwezesha barabara zote za Jiji la Dar es Salaam kupitika katika majira yote yam waka.
Prof. Mbarawa alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mradi huo utakelezwa kwa ufanisi, viwango na ubora wa hali ya juu na kuwahakikisha wananchi waliopitiwa na mradi huo kuwa barabara hizo zitamaliza kero ya muda mrefu ya msongamano wa magari na hivyo hawana budi kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa alisema tangu mwaka 1932 wakati wa utawala wa Gavana wa Kiingereza, Serikali iliweka sheria ya upanuzi wa barabara katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na kutambua ongezeko la idadi ya watu na msongamano wa magari ambayo ingekuwepo katika miaka ya sasa, hivyo zoezi la ubomoaji wa nyumba hizo ulikuwa haukwepeki.
“Katika kutekeleza mradi huu wa barabara za njia sita, majengo ya Serikali ikiwemo Ofisi za Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na Wizara ya Maji pia yameondolewa katika maeneo ya hifadhi ya barabara ambapo mradi huu utapita, hivyo nasi wananchi hatuna budi kuunga mkono juhudi hizi” alisema Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa alisema wakati wa utekelezaji wa mradi wa barabara hizo unaotarajiwa kujengwa katika kiwango cha lami, na hakutokuwa na usumbufu kwa wananchi wanaotumia barabara hizo kwani Serikali imejenga njia mbadala za pembezoni mwa Jiji ili kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale alisema Ofisi yake imejipanga kikamilifu kutekeleza mradi huo ili kuhakikisha kuwa Jiji la Dar es Salaam linaendelea kuwa kitovu cha uchumi na kiungo cha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi jirani.
Mhandisi Mfugale alisema katika kuondoa changamoto ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, Ofisi yake imeiweka barabara ya Ubungo-Kimara katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo yao.
Naye Mwananchi wa Kimara Temboni Jijini Dar es Salaam, Said Kilindo alisema wananchi wa maeneo hayo wamepokea kwa moyo mkunjufu utekelezaji wa mradi huo na kuiomba Serikali kutatua baadhi ya changamoto ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya vyoo katika maeneo mengi ya wafanyabiashara waliokuwepo katika maeneo hayo.
Comments