Kufuatia taarifa ya mashambulizi na mauaji ya walinda amani wa UN 14 na wengine 53 kujeruhiwa yaliyotokea katika Jimbo la Kivu, Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad ametuma salamu za rambirambi kwa Rais John Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali, Venance Salvatory Mabeyo, familia na ndugu wa marehemu na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao kwa niaba ya Tanzania.
“Tunaungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulaani shambulio hilo ambalo ni sawa na uhalifu wa kivita na kuitaka DR Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na wahusika wote kuchukuliwa hatua stahiki na kuwajibishwa,” amesema na kuongeza.
“Natuma salamu zangu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waathirika wote na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwa wale waliojeruhiwa nawatakia uponaji wa haraka ili warejee katika majukumu yao ya kawaida. Aidha, tunawaombea marehemu wote Mwenyenzi Mungu awapumzishe mahala pema peponi-Aamini.
Comments