Wakati bilionea mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite yanayopatikana Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, marehemu Erasto Simon Msuya (43) akitarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwao mtaa wa Kairo, Mji mdogo wa Mirerani, polisi imewatia mbaroni watu wawili wakihusishwa katika mtandao uliofanya mauaji ya mfanyabiashara huyo.
Marehemu Erasto Msuya enzi za uhai wake
Mfanyabiashara huyo anayemiliki vitega uchumi kadhaa katika miji hiyo, aliuawa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai baada ya kumiminiwa risasi zaidi ya 20 za bunduki ya kivita aina ya SMG.
Habari zilizopatikana jana Arusha, zilidokeza kuwa washukiwa hao walikamatwa siku ya tukio huko Sanyajuu wilayani Siha, kilomita chache kutoka mahali ilipotelekezwa pikipiki iliyotumika katika mauaji hayo.
Pikipiki hiyo mpya ilitelekezwa katika Kijiji cha Olkolili baada ya kupata pancha gurudumu la mbele na watu waliokuwa wakiitumia waliiacha na kuamua kutembea kwa miguu.
Habari zinadai kuwa watu hao wawili sio waliomfyatulia risasi mfanyabiashara huyo bali wana ‘taarifa muhimu’ zinazohusiana na mpango mzima wa mauaji hayo na mtandao wa watuhumiwa waliohusika.
Inadaiwa kuwa baada ya wauaji wa mfanyabiashara huyo kutelekeza pikipiki hiyo, ‘waliwezeshwa’ kutoroka kupitia Wilaya ya Simanjiro na baadaye kuingia jijini hapa ingawa hawajulikani mahali waliko.
“Ni kweli kuna watu wawili walikamatwa na wanashikiliwa kule Makao Makuu ya Polisi Moshi na kila siku wanaletwa hapa Arusha kwa ajili ya uchunguzi wa kuwatafuta wahusika hasa,” alidokeza polisi mmoja.
Comments