Waandishi wa habari nchini Tanzania wanakabiliwa na vitisho
vinavyoongezeka na ukosefu wa kulindwa na serikali, ambapo kumetokea kwa
uchache mashambulizi 10 dhidi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari tangu
Septemba 2012, ilisema Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ)
siku ya Jumanne (tarehe 6 Agosti).
"Licha ya heshima ya Tanzania kwa uwazi na demokrasia, raia wake
wananyimwa haki muhimu ya habari," ilionya CPJ. "Kuzuka kwa mashambulizi
dhidi ya waandishi wa habari, sheria za ukandamizaji wa vyombo vya
habari, kunapandikiza hisia za kujichuja wenyewe miongoni mwa waandishi
wa habari wa Tanzania, hasa wale wanaofanya kazi kwenye maeneo ya
vijijini."
Mashambulizi ya karibuni zaidi yanajumuisha kuuawa kwa mpiga picha Daudi
Mwangosi, aliyepigwa kwa bomu la machozi wakati akiripoti maandamano
mwezi Septemba, na kupigwa vibaya kwa mhariri Absalom Kibanda mwezi wa
Machi, ambapo alipofuliwa jicho na sehemu ya kidole chake kukatwa.
"Kuzorota kwa hali ya vyombo vya habari kumesadifiana na woga miongoni
mwa wanachama wa chama tawala wasiozoea kukosolewa na wasiojiandaa kwa
changamoto ya kisiasa," ilisema ripoti hiyo.
CPJ ilisema ingawa serikali ya Tanzania iliahidi kuzifanyia mabadiliko
sheria za vyombo vya habari, kuna mambo machache sana yaliyotekelezwa.
"Ukandamizaji wa serikali ya Tanzania dhidi ya uhuru wa habari na
kujieleza ni dalili ya wazi kwamba inahisi inatishiwa kwenye uchaguzi wa
urais na wabunge wa mwaka 2015," alisema mwandishi wa ripoti hiyo ya
CPJ, Tom Rhodes, kwa mujibu wa AFP.
Chanzo - sabahionline.com
Comments