LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho ameamua kuongeza kasi ya kumsajili mshambuliaji, Samuel Eto'o kutoka klabu ya Anzhi Makhachkala ya Russia.
Mourinho ameamua kumuongezea kasi baada ya mipango yake ya kumnasa mshambuliaji, Wayne Rooney kutoka Manchester United kukwama.
Kocha huyo kutoka Ureno amefikia uamuzi huo baada ya saa 48 alizotoa kwa Rooney, akimtaka aamue moja, kumalizika bila mchezaji huyo kutoa tamko lolote.
Mourinho alitoa saa 48 kwa Rooney ili aamue iwapo atabaki Manchester United ama atatua Chelsea.
Chelsea iliwasilisha ofa mara mbili kwa Manchester United ikitaka kumsajili Rooney, lakini mashetani hao wekundu wamekuwa wakigoma kumuuza mchezaji huyo.
Awali, Rooney alionyesha nia ya kutaka kuondoka Manchester United baada ya Kocha David Moyes kusema, chaguo lake la kwanza katika nafasi ya mshambuliaji wa kati ni Van Persie.
Mourinho amesema atakamilisha usajili wa mshambuliaji huyo wa Anzhi Makhachkala ndani ya saa 24 zijazo ili kujenga upya safu yake ya ushambuliaji.
Chelsea tayari imemsajili winga, Willian kutoka Anzhi na Eto'o ni mchezaji wa pili kufuata baada ya klabu hiyo ya Russia kukumbwa na mzozo wa kimasilahi.
Habari za awali, zimedokeza kuwa Eto'o anaweza kutia saini mkataba wa mwaka mmoja.
Nguli huyo aliwahi kufanya kazi na Mourinho katika klabu ya Inter Milan. Pia amewahi kuzitumikia klabu za Mallorca na Barcelona za Hispania.
Comments