Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni
mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini
Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.
Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge kumbana na
wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya washukiwa
pasi na ushahidi wa kutosha.
“Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa
kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na
jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna
vithibitisho.
“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha
maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli
ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema),
Mchungaji Israel Natse.
Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka
majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika
wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya
zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu
kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”
Comments