Waazimia kuunda timu ambayo itamshawishi January Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Morogoro. Viongozi wa Vyuo Vikuu 21
nchini wameazimia kwa kauli moja kuunda timu ndogo itakayokwenda
kumshawishi Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo
Kikuu Mzumbe tawi la Mbeya, Theonest Theophil alisema hilo ni moja ya
maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa siku mbili na kuwashirikisha
marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu na maspika wa vyuo 21 nchini.
Theophil alisema mkutano huo
uliyapigia kura majina matatu yakiwamo ya wabunge wengine wawili vijana;
John Mnyika na Zitto Kabwe na kwamba Makamba alipitishwa kuwa chaguo
lao baada ya kupata kura 70 kati ya 105 zilizopigwa. Alisema Zitto
alipata kura 20 na Mnyika kura tisa, huku kura tisa zikiharibika.
Alisema viongozi hao wamepanga
kutembea nchi nzima na kuwashawishi Watanzania kumuunga mkono Makamba
endapo ataafiki kuwania nafasi hiyo ya urais, huku wakidai kwamba
wamechoshwa na viongozi wenye visasi na uadui ambao wamekuwa wakitumia
muda mwingi kulumbana na kupambana badala ya kuwatumikia wananchi.
Theophil alisema mkutano huo ulilenga
kujadili mustakabali wa nchi katika masuala ya ubora wa elimu na
vihatarishi vya amani ambavyo vinatokana na chuki za kidini, siasa na
visasi. Pia walijadili tatizo la ajira kwa vijana, ukuaji wa uchumi na
mchakato wa Katiba Mpya ambao alisema hivi sasa ni kama umetekwa na
ushabiki wa kisiasa.
Theophili alisema walibaini kwamba ili
kukabiliana na changamoto zilizopo lazima nchi iwe na uongozi thabiti,
hivyo walimchagua Makamba kama mmoja wa viongozi wenye sifa za kushika
wadhifa wa urais kwa kuzingatia sifa alizonazo.
Alizitaja baadhi kuwa ni kuonyesha
uwezo na ujasiri katika nafasi za uongozi alizowahi kushika na uadilifu,
kwani hajawahi kuhusishwa na vitendo vya rushwa na ufisadi katika
uongozi wake.
Kwa upande wake, Said Ngolola kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu limekuwa likiathiri mfumo wa elimu ya juu nchini, kutokana na
kushindwa kwa waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo hali ambayo
imekuwa ikileta migogoro isiyoisha..
Mkutano wa viongozi hao uliandaliwa na
kufadhiliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya FPID inayojihusisha na
mapambano dhidi ya maradhi, ujinga na umaskini yenye makao yake makuu
Dar es Salaam.
Katibu wa asasi hiyo, Frances Ndunguru
alisema asasi hiyo haina uhusiano wowote na wanasiasa, bali lengo ni
kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kukutana na kujadili masuala
yenye masilahi kwa nchi.
CHANZO: mwananchi.co.tz
Comments