MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana wameonyesha nia yao ya kutetea taji hilo msimu ujao baada ya kuichapa Azam bao 1-0 katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo huchezwa kila mwaka kabla ya kuanza kwa ligi kuu, ikizikutanisha bingwa wa ligi ya msimu uliopita na mshindi wa pili.
Kipigo hicho kilikuwa ni mwendelezo wa ubabe wa Yanga kwa Azam baada ya msimu uliopita kushinda mechi zote mbili za ligi kuu. Katika mechi ya kwanza, Yanga ilishinda mabao 2-0 na katika mechi ya pili ilishinda bao 1-0.
Kiungo Salum Telela aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Didier Kavumbagu.
Yanga ilipata pigo dakika ya 11 baada ya beki wake kisiki, Kevin Yondani kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji John Bocco wa Azam. Beki huyo wa zamani wa Simba alitibiwa kwa dakika kadhaa, lakini alishindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikachukuliwa na Mbuyu Twite.
Yanga ilipata pigo jingine dakika ya 11 baada ya kipa wake, Ally Mustapha Barthez kuumia kufuatia kugongana na Kipre Tchetche wa Azam alipokuwa katika harakati za kuzuia mashambulizi kwenye lango lake. Nafasi yake ilichukuliwa na Deo Munishi 'Dida'
Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’/Deo Munishi ‘Dida’ , Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Salum Telela, Jerry Tegete/Hussein Javu, Didier Kavumbangu na Haruna Niyonzima.
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo, Waziri Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Himid Mao, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Gaudence Mwaikimba , Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha.Inatoka kwa mdau.
Comments