Na Victor Melkizedeck Abuso
Marekani inasema itachukua hatua dhidi ya Syria baada ya kutokea kwa
shambulizi la silaha za kemikali wiki iliyopita jijini Damascus na
kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa Mambo ya nje John Kerry amesema kuwa kilichotokea nchini Syria
hakikubaliki kamwe na ni lazima serikali ya rais Bashar Al Assad
iwajibike kwa mauaji hayo.
Marekani na washirika wake kama Ufaransa na Uingereza wanasema wakati
umefika kwa Syria kuvamiwa kijeshi pendekezo ambalo washirika wa karibu
wa rais Assad China na Urusi wanapinga.
Leo ni siku ya pili ya uchunguzi unaofanywa na watalaam wa Umoja wa
Mataifa kubaini ikiwa kweli silaha za kemikali zilitumiwa dhidi ya raia
wasiokuwa na wakati.
Rais Bashar Al Assad amesema kuwa tishio la Marekani kuwa ikiwa
uchunguzi utabaini kuwa silaha hizo zilitumiwa, italazimika kuingilia
mzozo huo kijeshi ni jambo ambalo halikubaliki kamwe.
Akihojiwa na gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia Assad amesisitiza
kuwa Marekani haitafaulu na kamwe hawezi kuwa kibaraka cha mataifa ya
Magharibi na ataendelea kupambana na makundi ya kigaidi yanayolenga
kuiangusha nchi yake.
Comments