Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo
Kenyatta umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini
Nairobi. Kwa sasa moto huo umeweza kudhibitiwa
Rais Uhuru Kenyatta amewasili katika
uwanja huo na anatarajiwa kuhutubia waandishi wa habari baadaye. Hadi
kufikia sasa hakuna ripoti zozote za majeruhi .
Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.
Mamlaka ya uwanja huo imesema kuwa tayari watu waliokuwa katika eneo hilo wameondolewa.
Imesema kuwa baadhi ya operesheni za
uwanja huo zimekatizwa huku ndege zinazoingia katika uwanja huo
zikielekezwa kutua katika viwanja vingine ndege kama vile Entebe, Dar es
Salam ,Kigali, Mombasa na kwingineko nchini Kenya.
Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia zimeahirishwa.
Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye
maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali
kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.
Huu ni moto mkubwa zaidi kuwahi
kushuhudiwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta wenye kutumiwa na wasafiri
wengi zaidi katika eneo la Afrika mashariki na kati .
Taarifa za awali zilionyesha kuwa moto
huo ulianzia kwenye eneo la uhamiaji katika kitengo cha kupokea wageni
kabla ya kusambaa hadi maeneo ya ushuru na mizigo ya abiria.
Chanzo cha moto huo bado
hakijajulikana , lakini maafisa wa ngazi ya juu wa serikali wakiongozwa
na rais Uhuru Kenyatta wametembelea uwanja huo na kutoa wito uchunguzi
ufanyike mara moja. Hata hivyo hawakutoa ishara yoyote ni lini uwanja
huo utafunguliwa tena .
Shirika la ndege la kenya -Kenya
Airways, ambalo ni kubwa zaidi katika kanda ya Afrika limefuta safari
zake zote na kuelekeza ndege zinazoingia nchini katika mji wa Mombasa .
Tayari hisa za ndege zimeshuka kwa kiwango cha asilimia 2 . Ndege za
kimataifa ambazo zilitakiwa kuondoka leo asubuhi ziliruhusiwa kuondoka
bila wasafiri.
Chanzo: BBC Swahili
Comments