Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi limeimarisha ulinzi kwenye maeneo ya ibada, fukwe za
bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote yatakayokuwa na
mikusanyiko mikubwa ya watu wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid el
Fitri.
Taarifa ya polisi iliyosainiwa na msemaji wa jeshi hilo, SSP Advera
Senso, pia imewataka wananchi kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za
haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu.
Alisema katika taarifa hiyo kuwa uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya watu
hutumia kipindi cha sikukuu kama mwanya wa kufanya uhalifu kutokana na
mikusanyiko watu.
Alisema polisi kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi
limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanasherekea sikukuu hiyo kwa
amani na utulivu, pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa
amani.
Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, aliwataka wamiliki
wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika
uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza
tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Pia amewataka wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto, ili
kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara.
Aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli yanayotumia majina ya
viongozi, watu maarufu na wafanyabiashara wakubwa kujipatia pesa na
vitu mbalimbali.
Alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia ujumbe mfupi wa simu za mkononi kupata taarifa za mtu binafsi hatimae mtu huyo kuibiwa.
Kuhusu agizo la Rais Kikwete la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha
sheria kusalimisha silaha zao, Senso alisema baadhi ya watu hao tayari
wameanza kusalimisha silaha hasa katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
Kuhusu wajamiaji haramu, alisema tayari wameanza kurudi makwao na kusema hiyo ni hatua nzuri.
Alitoa wito kwa watu hao kuendelea kutekeleza agizo la serikali kabla ya
operesheni kabambe kuanza itakayoendeshwa na polisi kwa kushirikiana na
vyombo vyengine vya ulinzi na usalama.
Chanzo - ZanziNew
Comments