Shambulizi la kujitoa mhanga lililotekelezwa nchini Syria limesababisha
watu 31 kupoteza maisha baada ya bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari
kulipuka katika Jiji la Damascus karibu na Makao makuu ya Chama cha
Baath.
Shambulizi la Bomu la Kujitoa Mhanga lililotekelezwa Jiji Damacus na kusababisha vifo vya watu 31
Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu yamethibitisha kutokea kwa
mashambulizi manne tofauti nchini Syria katika Jiji la Damascus
yanayotajwa kutekelezwa na Wapiganaji wa Upinzani.
Wengi wa waliopoteza maisha kati ya hao 31 ni raia wa kawaida ambapo
taarifa zinasema watu wengine wengi wamejeruhiwa bila ya kutajwa idadi
kamili ya wale waliopata majeraha kwenye mashambilizi hayo.
Shambulizi la bomu la kujitoa mhanga lililotekelezwa kwenye Makao Makuu
ya Chama tawala Cha Baath ndilo linatajwa kuchangia vifo vya watu wengi
zaidi huku mashambulizi mengine yakifanywa katika eneo la Mazraa.
Televisheni ya taifa inayounga mkono serikali ya Rais Bashar Al Assad
imesema mashambulizi hayo ni muendelezo wa mashambulizi ya kigaidi
yanayofanywa na wapinzani wa serikali.
Televisheni ya Al-Ikhbariya imeonesha baadhi ya video za shambulizi hilo
huku watu wengi wakionekana kuhaha huku na kule katika kuwaokoa
manusura wa shambulizi hilo katika Jiji la Damascus.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Ikhbariya miongoni mwa waliopoteza
maisha ni pamoja na watoto wanne waliokuwa karibu kabisa na Makao Makuu
ya Chama Tawala cha Baath huku wengine wakijeruhiwa.
Mashuhuda wa shambulizi hilo wamesema waliona gari moja likilipuka
kwenye kituo cha ukaguzi wa magari kilichopo karibu na Ubalozi wa Urusi
na Makao Makuu ya Chama Tawala Cha Baath.
Comments