MBUNGE wa Ubungo Jijini Dar es Salaam (Chadema), John Mnyika amemtaka,
Rais Jakaya Kikwete kutosaini marekebisho ya sheria mpya ya mabadiliko
katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008.
Mnyika pia anakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne
Makinda kwa kutumia vibaya kanuni za Bunge kutokana na kitendo chake
cha kuzivunja kamati tatu za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC).
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, jana, Mnyika alisema Rais Kikwete
kabla ya kusaini marekebisho hayo ambayo yanaonyesha dalili za kuwalinda
mafisadi, ajitokeze na kuwaeleza Watanzania faida na hasara ya
mabadiliko ya sheria hiyo.
Wiki hii Serikali iliwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko katika
Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu
ambavyo vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Marekebisho hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria,
namba tatu wa mwaka 2012 uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema.
Marekebisho hayo yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa kushughulikia
taarifa hiyo, kwani yanaongeza vipengele, vinavyoliwajibisha Bunge kwa
Serikali.
Serikali imeongeza vipengele vya ziada ambavyo vinazitaka kamati za
Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa
Serikali ili yatafutiwe majawabu badala ya utaratibu wa sasa wa
kupeleka hesabu zake bungeni.
Comments