UCHAGUZI wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
uliofanywa na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho Jumatatu wiki hii
mjini Dodoma, ni kama unabadili mwelekeo wa siasa za ndani za chama
hicho kikongwe nchini.
NI DK SALIM,NCHIMBI,MWINYI,MIGIRO NA WASSIRA
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka saba iliyopita na
kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa kwenye minyukano
ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na utulivu wa kisiasa
kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya
kiuongozi.
Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu umeweka kando baadhi
ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa katika harakati za
kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza sura mpya ambazo
huenda baadhi yao wanaweza kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kupiga
mbio hizo, lakini waliwekwa kando katika Kamati Kuu ya sasa.
Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano Profesa Mark
Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli (Ujenzi), Dk
Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin
Shigela, pia hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia katika CC
ambacho ni chombo cha kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.
Comments