WAMSUSIA MEYA, WATUMA UJUMBE MZITO KWA MANGULA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Bukoba Mjini, kimeingia katika
siasa chafu za kudhalilishana huku vipeperushi vya kuwatusi madiwani 10
wa chama hicho na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) vikisambazwa mitaani.
Madiwani hao waliochafuliwa kwa matusi mazito ya nguoni ambayo mengine
hayaandikiki kwa kuzingatia maadili ni wale nane wa CCM akiwemo Mbunge
wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, na wawili wa CUF waliosaini
hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura
cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Anatory Amani anayekabiliwa na
tuhuma za ufisadi.
Hatua hiyo inakuja siku chache tangu Dk. Amani aamue kupuuza maagizo ya
Makamu Mwenyekiti wao chama hicho taifa, Philip Mangula, kwa kufungua
kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na kung’olewa na madiwani.
Mangula ambaye alilazimika kufika mjini Bukoba mwezi uliopita ili
kunusuru mtafaruku huo, aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa
wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili
zipatiwe ufumbuzi.
Lakini katika hatua ambayo imetafsiriwa kuwa mgogoro huo unazidi kushika
kasi, juzi vipeperushi hivyo vya matusi vilisambazwa na watu
wasiojulikana kwa kuvibandika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bukoba.
Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya
huyo mbali na Kagasheki ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya
Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Bukoba.
Comments