Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa,
|
WAKATI mjadala wa kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato
cha nne ukiendelea nchini, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa,
amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume kuchunguza na kutoa mapendekezo
ya mfumo bora wa elimu nchini.
Alisema kwa hali ilivyo sasa mtu mmoja hawezi kujifungia ofisini peke
yake na kuja na mfumo wa kuboresha sekta ya elimu utakaokidhi matakwa ya
jamii.
Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.
Ingawa hakutaka kuzungumzia hoja ya mbunge wa kuteuliwa na Rais, James
Mbatia (NCCR- Mageuzi), aliyetaka Bunge liunde kamati kuchunguza udhaifu
katika sekta ya elimu na hoja hiyo kutupwa, Lowassa alisema hakuna
sababu ya kubishana kama tuna mitaala au la, lakini jambo la msingi ni
kuhakikisha tunapata sababu za matokeo mabaya ya wanafunzi wa kidato cha
nne.
“Sitaki kuzungumzia mjadala wa bungeni huyo anasema hatuna mitaala,
serikali inasema tunayo, hoja ya msingi zaidi ni kuangalia hii mitaala
ni sahihi, inatufaa? Mfumo wetu wa elimu ni mzuri?” alisema Lowassa na
kuongeza kuwa tume itakuja na majibu kama mitaala yetu ni sahihi na kama
inatufaa au la.
Akitolea mfano, Lowassa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, Waziri wa
Elimu wakati huo, marehemu Jakson Makweta, aliunda tume kuchunguza mfumo
wa elimu na ilikuja na majibu mazuri yaliyofaa kwa wakati ule na sasa
tunahitaji tume nyingine kuja na majibu ya wakati uliopo.
“Miaka ya nyuma, Rais Reagan wa Marekani wakati huo, aliunda tume
kuchunguza ubora wa elimu inayotolewa nchini mwake na tume hiyo ilikuja
na majibu yaliyofanyiwa kazi na leo hii Marekani ina mfumo mzuri na bora
wa elimu,” alisema Lowassa.
Comments