Na Victor Melkizedeck Abuso
Mataifa yenye nguvu duniani yamelaani hatua ya Korea Kaskazini kujaribu
zana zake za Nyuklia licha ya onyo la kutofanya hivyo kutoka kwa Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Marekani,China na Urusi ambayo
kwa pamoja viongozi wake wameungana kukashifu hatua hiyo ya Pyongyang,
na kutaka ichukuliwe hatua ya kuwekewa vikwazo zaidi.
Korea Kaskazini inasema imefanikiwa kufanya jaribio la ardhini la zana
zake za Nyuklia na kuzua shutuma nzito kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Serikali ya Pyongyang inasema jaribio hilo la tatu limefanikiwa pakubwa sana na limefanyika kwa utalaam wa hali ya juu.
Rais wa Marekani Barrack Obama ameshtumu hatua hiyo ya Korea Kaskazini
na kusema kuwa ni sharti Jumuiya ya Kimataifa ichukue hatua dhidi ya
serikali hiyo kwa kile alichokieleza hatua hiyo inatishia usalama wa
Marekani na wa dunia nzima.
Awali, Umoja wa Mataifa ulikuwa umeonya serikali ya Pyongyang kuwa
itachukuliwa hatua ikiwa itafanya jaribio lingine la zana zake za
Nyuklia.
Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameshtumu hatua hiyo
anayosema imevunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa
kufanya jaribio hilo.
Wajumbe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana siku ya
Jumanne kujadili hatua hiyo ya Pyongyang na kuona ni hatua gani
watakayochukua dhidi ya serikali hiyo.
Comments