CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimeendelea na mchakamchaka wake
ulioanzia bungeni wa kutaka hoja zake zisikilizwe baada ya kutupiliwa
mbali kimizengwe bungeni.
Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mboye
Wabunge wa upinzani waliowasilisha hoja zao ni pamoja na Mbunge wa
Kuteuliwa, James Mbatia aliyetaka mfumo wa elimu nchini ufumuliwe au
kuboreshwa.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
alitetea mfumo wa elimu uliopo kabla ya hoja hiyo kuondolewa kabisa.
Hoja nyingine ni kero ya maji jijini Dar es Salaam iliyotolewa na Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika ambayo nayo iliondolewa baada ya Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe kueleza kuwa Serikali inaendelea kutatua
tatizo la mbunge huyo.
Hali hiyo ilizua vurugu na matokeo yake hoja nyingine binafsi za
wabunge, ikiwamo ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari aliyetaka
kujadiliwa kwa mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa na jinsi
linavyoathiri mfumo wa elimu nchini, ziliahirishwa kwa muda
usiojulikana.
Mbali na kuzitupilia mbali hoja hizo, Bunge hilo lilimalizika likiifuta
Kamati ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Baada ya wabunge hao kuvutana bungeni, wameamua kufanya maandamano na
mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam ili kuwaeleza wananchi
kilichotokea Bungeni na kuweka mikakati zaidi.
Mkakati wa kumng’oa Spika
Katika mkutano wa hadhara, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara),
Zitto Kabwe anasema Spika wa Bunge, Anna Makinda ameshindwa kuwajibika
na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye
kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta (Poac), Zitto aliyekuwa
Mwenyekiti wa kamati hiyo, anasema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima
sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia maslahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Zitto
anataja mbinu ya kwanza ya kumng’oa spika kuwa ni kuwasilisha hoja ya
kutokuwa na imani naye, ambayo imeshakamilika inasubiri wakati wake.
“Njia ya pili tuandamane hadi pale shule ya msingi Bunge… au tutumie
namba zake (za simu) kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…”
anasema Zitto.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto anataja sababu ya kufutwa
kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya
zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika
katika kampeni za CCM, na ujenzi wa vyuo vikuu vya Dodoma, Hombolo na
Chuo Kikuu cha Arusha Nelson Mandela.
“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi
tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima
adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” anasema Zitto.
Zitto aligusia pia sakata la Mtwara akisema kamati iliyofutwa ililitaka
Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) kuonyesha mkataba wa ujenzi wa
bomba la mafuta, wakaahidi kuupeleka ifikapo Aprili mwaka huu.
“Tulipowataka TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi wakasema
uko wizarani. Katibu Mkuu ambaye anapaswa kwenda kujieleza kwenye
Kamati ya Nishati na Madini hakwenda kwa kuwa kamati hiyo pia imefutwa.
TPDC wakasema watauleta Aprili. Ndiyo hivyo kamati yetu nayo imefutwa.”
Chanzo; Gazeti la Mwananchi
Comments