Israel imeonyesha ishara kwamba ilifanya
mashambulizi ya anga nchini Syria wiki iliyopita, huku Rais Bashar
al-Assad akilituhumu taifa hilo la Kiyahudi kwa kujaribu kuidhoofisha
nchi yake ambayo inakumbwa na vita.
Israel imeonyesha ishara japo sio wazi kwamba ilifanya mashambulizi ya
anga nchini Syria juma lililopita, huku Rais Bashar al-Assad akilituhumu
taifa hilo la Kiyahudi kwa kujaribu kulidhoofisha taifa lake hilo
ambalo linakumbwa na vita.
Siku nne baada ya Syria kudai kuwa Israel inahusika na shambulio la anga
katika kituo cha utafiti wa kijeshi karibu na mji mkuu wa Damascus,
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak, amezungumza na waandishi wa
habari mjini Munich, Ujerumani, lakini ameshindwa kuthibitisha kwamba
Israel inahusika na shambulio hilo.
Kiongozi wa Hizbollah, Hassan Nasrallah
Barak jana aliwaambia wanadiplomasia wa ngazi za juu na maafisa wa
masuala ya ulinzi katika mkutano wa usalama mjini Munich kwamba hicho
kilikuwa ni kithibitisho kwamba wanaposema kitu huwa wanamaanisha.
Israel haijathibitisha rasmi kuhusika na shambulio hilo, ingawa imekuwa
ikizituhumu Iran na Syria kwa kulipatia silaha kundi la Hizbollah ambalo
lilipambana na Israel katika vita vya mwezi mmoja mwaka 2006.
Barak amesema hawadhani kama Syria inaruhusiwa kupeleka silaha za kisasa Lebanon.
Syria yatishia kulipiza kisasi
Syria imetishia kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi hayo
yaliyofanywa Jumatano iliyopita. Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip
Erdogan mkosoaji mkubwa wa Assad na Israel ameituhumu Israel kwa
kuendeleza hali ya ugaidi ambapo amelaani shambulio hilo la anga akisema
halikubaliki na linakiuka sheria za kimataifa na amekiita kitendo hicho
ni uchokozi wa kigeni. Aidha, ameikosoa Iran kwa kuiunga mkono Syria.
Comments