Elias Msuya, Zanzibar na Daniel Mjema, Moshi
ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao na ndugu wa
marehemu wa Padri Evarist Mushi wameitupia lawama Serikali kwa kuzembea
kuwalinda viongozi wa dini hiyo waishio Zanzibar licha ya kupewa
taarifa za viashiria vya hatari mara kwa mara.
Askofu wa Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kadinali Pengo
Askofu Shao alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
Zanzibar na ndugu wawili wa Padri Mushi walieleza hayo huko Moshi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema
jana kwamba hawajapata malamamiko yaliyoelezwa na Askofu Shayo na kwamba
kama Rais Jakaya Kikwete angeyapata asingeacha kuyashughulikia.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa naye alikanusha madai hayo akisema:
“... Hapa tulipo tuna kesi nyingi na kuna watu wanahojiwa. Sisi
hatufanyi kazi kwa shinikizo la mtu, kama ni hivyo vipeperushi hata sisi
tunavipata siyo wao tu. Sasa tutawakamataje wakati watu wenyewe
hatuwajui?”
Hata hivyo, Askofu Shao alisema hawaridhishwi na utendaji kazi wa Polisi
na kudai kwamba Wakristo wa madhehebu yote wanalengwa na mashambulio
yanayofanywa na watu aliosema kuwa wanapata msaada kutoka nje.
“Niseme wazi tu, haturidhishwi na utendaji wa Serikali katika kutulinda.
Tumemwandikia barua Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein na Rais
Jakaya Kikwete tukiwaeleza vitisho tunavyopewa, lakini hatuoni hatua
zikichukuliwa,” alisema Askofu Shao na kuongeza:
“Walipomshambulia Padri Ambrose Mkenda watu hao walileta ujumbe kwamba,
tumeshawaweza Padri Ambrose na Sheikh Fadhil Soraga na bado tutaendelea.
Vijana wetu wa kazi wameshamaliza mafunzo Somalia,” alinukuu moja ya
kipeperushi huku akisema kuwa tatizo la Serikali ni kutokuwajibika.
Comments