Skip to main content

Warioba: Katiba ya Tanganyika inawezekana kwa miezi mitatu


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba ya Tanganyika inaweza kuandikwa ndani ya miezi mitatu tu kwa kuwa maoni mengi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa Jumatatu, kwa kiwango kikubwa yametoka kwa wananchi wa upande huo wa Muungano.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akizungumza katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao
Warioba alisema hayo jana wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
“Kutunga Katiba ya Tanganyika siyo kazi ngumu, ukisoma rasimu hii sura ya kwanza mpaka ya tano, sioni kama Katiba ya Tanganyika itakuwa tofauti na maoni yaliyomo katika sura hizo,” alisema na kuongeza:
“Misingi iliyopo katika utangulizi wa rasimu hii imetokana na maoni ya wananchi hao. Wakati wa kukusanya maoni, Zanzibar walijikita zaidi kwenye Muungano, maoni mengine kwa kiwango kikubwa yametoka kwa Watanzania Bara na katika kuandika Katiba ya Tanganyika sioni kama watabadilisha chochote kuhusu misingi hii ambayo ni; tunu za taifa, maadili, malengo na haki za binadamu.”
Alisema kuhusu kubadilishwa kwa mihimili ya Serikali na vyombo vingine vya kitaifa, kikubwa kinachoweza kuguswa ni muundo wa Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Baraza la Mawaziri.
“Kuhusu taratibu za kufanya kazi; iwe ni madaraka ya Rais, utaratibu wa kufanya kazi katika Bunge, Mahakama na Serikali sioni kama litakuja suala jipya kwa sababu mambo hayo yameshatolewa maoni. “Kilichobaki ni madaraka kwa umma tu, kwa maana ya Local Government (Serikali za Mitaa).

Hata hili la madaraka kwa umma watakaolishughulikia watumie taarifa za wananchi waliotoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Wananchi walitoa maoni kuhusu jambo hili ambayo yapo wazi kabisa.”


Comments