Mauaji yatikisa nchi ya Misri wakati ikiadhimisha miaka mitatu ya mapinduzi yaliyoangusha utawala wa Hosni Mubarak
Waandamanaji wanaounga mkono serikali ya mpito wakiwa na picha za Mkuu wa Jeshi, Generali Abdel Fattah al-Sisi. Reuters/路透社 |
Na Flora Martin Mwano
Takribani watu 29 wameuawa katika ghasia baina ya waandamanaji na polisi
nchini Misri wakati Taifa hilo likiadhimisha kumbukumbu ya miaka mitatu
ya mapinduzi yaliyoangusha utawala wa Rais wa zamani wa Misri Hosni
Mubarak.
Wizara ya afya imesema watu wengine 168 wamejeruhiwa kutokana na ghasia hizo.
Wakati ghasia hizo zikiendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Misri, jijini
Cairo katika medani ya Tahrir wafuasi wa serikali ya mpito waliendelea
kushangilia miaka mitatu ya mapinduzi na kubeba mabango yenye ujumbe wa
kumuunga mkono Mkuu wa Jeshi Generali Abdel Fattah al-Sisi ambaye huenda
akawa Rais ajaye wa Taifa hilo.
Polisi walikabiliana nawaandamanaji wa kiislamu wanaopinga serikali ya
mpito ya kijeshi huku wakimuunga mkono Rais aliyepinduliwa mwezi Julai
mwaka jana Mohammed Morsi.
Hali ya usalama imezidi kuwa tete nchini humo kutokana na mashambulizi
ya mara kwa mara kujitokeza hususani katika vituo vya polisi, hivi
karibuni kundi la Ansar Beit al-Maqdis lenye uhusiano na mtandao wa
kigaidi wa Al-Qaeda limejigamba kutekeleza mashambulizi hayo.
Wizara ya mambo ya ndani inasema waandamanji zaidi ya 1000 wanashikiliwa kwa tuhuma za kufanya vurugu.
Polisi ambao pia wanatuhumiwa kuwauawa mamia ya waandamanaji wa kiislamu
toka kupinduliwa kwa Morsi wameapa kuendelea kuwadhibiti waandamanaji
hao wanaotuhumiwa kukiuka sheria za nchi hiyo.
Via kiswahili.rfi.fr
Comments