Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekataa kuidhinisha muswada wa kupiga
marufuku ndoa za watu wenye jinsia moja katika nchi hiyo ya Afrika
Mashariki.
Kama ungeidhinishwa muswada huo ungetoa adhabu kali kwa watu
wanaojihusisha na ngono za jinsia moja. Rais Museveni amemuandikia barua
Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga na kumkosoa kwa hatua ya kupitisha
muswada huo Disemba mwaka jana bila ya kuwa na idadi ya kutosha ya
Wabunge.
Aidha Rais Museveni amedai kuwa, watu wanaojihusisha na ndoa za jinsia
moja wana akili timamu na wanaweza kuokolewa kutokana na tabia hiyo
badala ya kuuawa au kufungwa jela.
Mswada huo unatoa adhabu kali kwa watu watakaopatikana na hatia ya
kufanya liwati na usagaji ikiwemo ya kufungwa jela maisha. Muswada huo
pia unaeleza kuwa, mtu yeyote aliyekuwa na taarifa za watu wanaoshiriki
ngono za watu wa jinsia moja na kushindwa kutoa taarifa hizo kwenye
vyombo husika atafungwa jela maisha.
Kwa mujibu wa gazeti la Monitor, Rais Museveni amesema kwamba, licha ya
kuwashauri wabunge kusubiri hadi serikali itakapoutathmini lakini
muswada huo ulishinikizwa zaidi na kupasishwa.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, pingamizi hilo la Rais Museveni
linachelea mashinikizo ya madola ya Magharibi ambayo baada tu ya
kupasishwa muswada huo bungeni yamekuwa yakiiandama nchi hiyo.
Chanzo: kiswahili.irib.ir
Comments