Watuhumiwa wanne wa shambulio la Westgate, Nairobi nchini Kenya
Mahakama ya Kenya leo imeanza kusikiliza kesi inayowakabili watuhumiwa
wanne wanaohusishwa na kundi la kigaidi la al Shabab ambalo lilitekeleza
shambulio dhidi ya jengo la maduka ya biashara la Westgate, Nairobi
nchini Kenya mwaka uliopita.
Mahakama hiyo imeanza kwa kusikiliza maelezo ya mlinzi ambaye alikuwa
nje ya jengo hilo wakati wa kutokea shambulio hilo tarehe 21 Septemba
mwaka 2013. Shambulio hilo lilisababisha mauaji ya watu 67 na makuni ya
wengine kujeruhiwa.
Taarifa kutoka Nairobi zinasema kuwa, Adan Mohamed Ibrahim, Muhammad
Ahmed Abdi, Liban Abdullah Omar na Hussein Hassan Mustafa ambao wote ni
raia wa Somalia, wanatuhumiwa kwa kushiriki kwenye shambulio hilo.
Watuhumiwa hao wamekanusha tuhuma za kushiriki kwao kwenye shambulio
hilo. Kundi la kigaidi la al Shabab lilitangaza kuhusika na shambulio
hilo lililochukua muda wa siku nne mtawalia.
Kundi hilo lilitangaza kuwa, shambulio hilo lilifanyika kwa ajili ya
kulipiza kisasi uingiliaji wa kijeshi wa Kenya kwenye eneo la kusini mwa
Somalia.
Comments