Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, vitalazimika kufanya mabadiliko katika safu zake za
uongozi kutokana na athari zilizosababishwa na mabadiliko yaliyofanywa
na Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Mawaziri.

Rais Jakaya Kikwete akimuapisha Jenister Mhagama kuwa Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya
Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman
Juzi, Ikulu ilitangaza mabadiliko katika baraza hilo ambayo yaliwaweka
kando mawaziri na manaibu waziri watano, huku sura kumi mpya zikiingia,
mabadiliko ambayo yameacha nafasi mbili wazi katika sekretarieti ya CCM
na nafasi nne katika uongozi wa Bunge.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa jana ni waliokuwa wajumbe wa
Sekretarieti ya CCM; Dk Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa kuwa Waziri
wa Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba ambaye ameteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Fedha.
Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, wakati Dk Migiro ni
Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alisema jana kuwa
viongozi wa sekretarieti ya CCM wanapoteuliwa kushika nafasi nyingine za
Serikali, wanalazimika kuziacha nyadhifa zao katika chama.
Nape alisema kwa maana hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete atalazimika
kuteua watu wa kuziba nafasi za Dk Migiro na Nchemba. “Huu ni utaratibu
tuliojiwekea katika chama kwamba viongozi wa sekretarieti hawatafanya
kazi mbili za chama na Serikali, kwa hiyo viongozi hawa pia wataziacha
nafasi za chama,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape alisema utaratibu huo hauwagusi wenyeviti wa chama hicho
wa mikoa, ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ama manaibu waziri kwani
uenyekiti si nafasi ya utendaji.
Katika uteuzi huo, Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani
aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wakati
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi aliteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Hawa wanaweza kuendelea na nyadhifa zao za uenyeviti katika chama, huku
wakiwa na nyadhifa serikalini, hii haina athari kwa sababu siyo
watendaji wakuu wa chama,” alisema Nape.
Comments