Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi, Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar linamshikilia Askari mmoja wa Chuo cha Mafunzo
kwa tuhuma za wizi wa shilingi 1,635,000 alizoziiba kutaka katika duka
moja lililopo eneo la Makadara mjini Zanzibar.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Mkadam Khamis
Mkadam, amemtaja Askari huyo kuwa ni Sajin Meja (S/Sgt) Hassan Iddi
Hassan (45), wa Chuo cha Mafunzo Makao Makuu.
Kamanda Mkadam amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11.00
jioni ambapo Askari huyo akiwa amevaa kiraia, alifika dukani hapo kama
mteja wa kawaida na wakati muuzaji wa duka hilo akimhudumia mteja
mwingine upande wa pili, aliingia ndani na kukimbilia kwenye droo ya
pesa na kuzichukua fedha hizo na kuondoka.
Amesema wakati akichukua fedha hizo, Askari huyo alionwa na baadhi ya
wateja na hivyo kumshitua muuzaji huyo na kuanza kupiga kelele za mwizi
na ndipo alipofukuzwa na wananchi na kwa vile eneo hilo lilikuwa karibu
na Kituo cha Polisi askari waliwahi haraka na kumkamatwa kabla ya kupata
kipigo kikali kutoka kwa wananchi.
Kamanda Mkadam, amesema fedha zote alizokua ameziiba mtuhumiwa huyo
zimeokolewa na Polisi na zimehifadhiwa kama kielelezo mahakamani.
Comments