Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeripoti kuwa limegundua na
kuzika maiti za watu 50 katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Jamhuri
ya Afrika ya Kati.
Taarifa iliyotolewa jana na Shirika la Msalaba Mwekundu ilisema kuwa
maiti hizo za watu waliouawa zilipatikana katika maeneo ya Bossembele,
Boyali na Boali.
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati Georgios Georgantas amesema kuwa wakazi wa maeneo hayo
hawana ulinzi wa aina yoyote na wanalazimika kukimbia makazi yao kwa
hofu ya kushambuliwa na makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha.
Jumuiya zisizo za serikali zinazofanya kazi katika maeneo hayo zinasema
kuwa hali ya wakazi wa maeneo hayo ni mbaya sana na kwamba ni maafa
yasiweza kudhibitiwa.
Maeneo mengi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yangali yanashuhudiwa wimbi
kubwa la mauaji yanayofanywa dhidi ya raia licha ya askari wa kulinda
amani wa kimataifa kuimarisha usalama wa kiwango fulani katika mji mkuu
wa nchi hiyo Bangui.
Comments