RAIS Jakaya Kikwete ameshauriwa katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza
la Mawaziri kumtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo kujieleza kwake na umma ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa
dhidi yake kutokana na ongezeko la bei ya umeme.
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (CHADEMA)
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Waziri Kivuli
wa Nishati na Madini, John Mnyika (CHADEMA), Rais Kikwete anapaswa
kutambua kuwa Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka
2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kuwa bei ya umeme haitapanda
hata baada ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwasilisha mapendekezo
ya kupandisha bei ya nishati hiyo.
Alisema kinyume na kauli za Prof. Muhongo, Bodi ya Wakurugenzi wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), katika kikao
cha Desemba 10, mwaka jana, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme
kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, hatua ambayo
itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa
nchi.
Wakati Mnyika akisema hayo, wananchi wamependekeza kwamba iwapo mamlaka
husika hazitapunguza kiwango cha ongezeko la bei ya umeme; maandamano
yaandaliwe kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za kunusuru
uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko hilo.
Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa uamuzi wa kupandisha
nishati hiyo ulifikiwa Oktoba 11, mwaka jana, baada ya TANESCO
kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Ewura, iliyopendekeza
kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia Oktoba 1, mwaka jana, asilimia
12.74 kuanzia Januari 1, mwaka huu na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1,
mwaka 2015.
Comments